Mifuko mbadala ya plastiki kukutanisha wadau

Muktasari:

  • Ofisi ya Makamu Rais (Muungano na Mazingira) yawaita pamoja wadau wa uzalishaji, usambazaji na wauzaji wa mifuko mbadala, ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu Kassim Majaliwa la kupiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki ifikapo Juni Mosi.

Dar es Salaam. Ofisi ya Makamu Rais (Muungano na Mazingira) imeandaa kikao maalumu na wazalishaji wa mifuko mbadala ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kupiga marufuku mifuko ya plastiki ifikapo Juni Mosi.

Majaliwa alitoa agizo hilo Aprili 9 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja za wabunge walizozitoa wakati mjadala wa bajeti ya ofisi ya waziri mkuu ya mwaka 2019/20.

 “Ifika Mei 31, mwaka huu itakuwa ni mwisho kutumia mifuko ya plastic kubebea bidhaa mbalimbali. Kuanzia sasa tunatoa fursa ya viwanda kubadili teknolojia yao, wauzaji kuondoa mizigo yao au kumaliza kuuza yote na kadhalika,” alisema.

Majaliwa alisema ofisi ya Makamu wa Rais itajiandaa kutumia kanuni chini ya Sheria ya Mazingira ili kulifanya katazo hilo kuwa na nguvu kisheria na kwamba hatua hizo zimechukuliwa ili kulinda afya ya jamii, wanyama, mazingira na miundombinu.

 Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na ofisi ya Makamu wa Rais, imeeleza kuwa kikao hicho kitafanyika Aprili 15 jijini Dar es Salaam.

 ‘Katika kutekeleza agizo la waziri mkuu tunawaalika wadau wote wanaojihusisha na uzalishaji, uuzaji na usambazaji wa mifuko mbadala kushiriki kikao hiki. Kikao hiki kitaongozwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira, January Makamba ,” ameeleza taarifa hiyo.