Mifuko ya ice cream, karanga marufuku

Thursday June 13 2019

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (Nemc), limeongeza wigo wa makali ya katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki kwa kupiga marufuku vifungashio vya kienyeji vinavyotumika kufungashia karanga, ice-cream, miwa na ubuyu na kwamba atakayekutwa navyo atalipa faini kati ya Sh30,000 na Sh200,000.

Marufuku hiyo, ilitangazwa jana na mkurugenzi mkuu wa Nemc, Dk Samuel Gwamaka wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Alisema vifungashio hivyo vya kienyeji haviruhusiwi kwa sababu havina vigezo wala viwango vilivyothibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Dk Gwamaka alifafanua kuwa vifungashio vilivyoruhusiwa ni vilivyopitishwa na kuthibitishwa na TBS na watengenezaji au wazalishaji wanaoweka alama na nembo maalumu kwenye vifungashio hivyo.

“Kuna bidhaa kama dawa ambayo kifungashio chake kinakuwa na nembo maalumu. Lakini siyo mfuko huu (anauonyesha) hauna nembo wala alama yoyote na haijulikani inatoka wapi na muagizaji au mtengenezaji ni nani?

“Haturuhusu na haturudi nyuma tutawakamata wengi, sasa kama wewe utaendelea kutumia mifuko hii tutakukamata kwa sababu mifuko mbadala ipo,” alisema Dk Gwamaka.

Advertisement

Alisema kuanzia leo atakayekutwa na kifungashio cha mifuko wa plastiki laini chenye rangi nyeupe amebebea bidhaa, atalazimika mfukoni kuwa na kati ya Sh30,000 hadi Sh200,000 kwa ajili ya kulipa faini au kupelekwa mahabusu kwa siku saba.

Juni Mosi, katazo la Serikali la matumizi ya mifuko ya plastiki lilianza kutumika baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kutangaza bungeni Aprili 9, kuwa mifuko ya plastiki hairuhusiwi.

Baada ya katazo hilo, kuanza kutumika Watanzania walitii na kuachana na mifuko hiyo, lakini badala yake wakaibukia kwenye matumizi ya vifungashio vya mifuko ya plastiki laini ambavyo navyo haviruhusiwi kwa sababu havikidhi viwango vya TBS.

Dk Gwamaka alisisitiza “hivi vifungashio vya namna hii vinaturudisha kule tulikotoka. Watanzania wajue kwamba vifungashio vinavyohitajika ni vile vilivyokidhi kiwango.”

“Kuanzia kesho (leo), tutakuwa mtaani, kuwafahamisha wananchi kuhusu jambo hili tumeona katazo lililotolewa na Serikali bado halijaeleweka kesho. Tutawafahamisha vifungashio vinavyohitaji kutumika”.

Mwanasheria wa Nemc, Manchare Heche alisema sheria na kanuni za katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki zipo wazi, mtu atakayekiuka hatua kali zitachukuliwa kama ilivyoanishwa katika kanuni ya nane za usimamizi wa mazingira za kupiga marufuku mifuko hiyo.

“Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ina viwango vilivyowekwa katika vibebeo na vifungashio inayoeleza unene na sifa zinazotakiwa. Kwa hiyo Nemc tunasubiri TBS iweke viwango hivi, tutakuwa na msako mkali utakaofanyika maeneo mbalimbali kwa watumiaji , wasambazaji na watengenezaji na tutakwenda sokoni na mabuchani,” alisema Heche.

Advertisement