Mikakati mipya ni muhimu CUF kukwepa njia iliyopitia NCCR-mageuzi

Muktasari:

Lakini tukio la sasa la kuhama kwa Maalim Seif kutoka CUF kwenda ACT-Wazalendo linaweza kufananishwa na lile lililotokea mwaka 1999 pale aliyekuwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema alipokihama chama hicho na kujiunga na TLP anayoiongoza hadi sasa.

Miaka miwili iliyopita Mwananchi liliwahi kufanya uchambuzi kuhusu vuta nikuvute ya mgogoro wa CUF kati ya aliyekuwa katibu mkuu wake, Maalim Seif Sharif Hamad na mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba.

Uchambuzi huo uliochapishwa mwaka 2017 ulipendekeza mambo kadhaa ambayo Maalim Seif anaweza kuyafanya kama njia ya kuhakikisha anaendeleza harakati za kisiasa kutokana na hali iliyokuwapo. Moja ya mapendekezo ilikuwa ni kuhamia chama kingine na ndiyo njia aliyoichagua.

Tukio la Maalim Seif kujiunga na chama cha ACT Wazalendo, juzi, linakumbusha mlolongo wa wanasiasa kuhama chama kimoja kwenda kingine kwa ajili ya kuhakikisha wanatimiza matarajio yao ya kisiasa.

Miongoni mwa matukio ya wanasiasa kuhama chama yaliyovuta wengi ni pamoja na lile la Profesa Kigoma Malima aliyetoka CCM kwenda NRA, Edward Lowassa kutoka CCM kwenda Chadema (2015) na wengineo.

Lakini tukio la sasa la kuhama kwa Maalim Seif kutoka CUF kwenda ACT-Wazalendo linaweza kufananishwa na lile lililotokea mwaka 1999 pale aliyekuwa mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, Augustino Mrema alipokihama chama hicho na kujiunga na TLP anayoiongoza hadi sasa.

Kujiunga NCCR, kuondoka

Mrema aliyeanzia siasa CCM ambako alishika nyadhifa mbalimbali ikiwamo ya waziri wa mambo ya ndani, naibu waziri mkuu na waziri wa kazi na maendeleo ya vijana, anatajwa kuwa ndiye kiongozi wa upinzani aliyeweka historia ya kuwa na kundi kubwa la wafuasi wakati huo na kukipasua kichwa chama tawala.

Alijiunga na NCCR mwanzoni mwaka 1995 wakati nchi ikielekea katika uchaguzi wake wa kwanza uliohusisha vyama vingi vya siasa na kuzua gumzo.

Baada ya kutangaza kuihama CCM, maelfu ya watu wakamfuata wengine wakiwa ni kutoka CCM na hata wale ambao hawakuwa na vyama au kutoka vyama vingine vya upinzani.

Licha ya kuwa kilikuwa kimefikisha miaka takribani mitatu tangu kusajiliwa, kabla ya Mrema kujiunga, NCCR haikuwa na umaarufu mkubwa na haikuwa na viongozi wa kuchaguliwa na wananchi kwa kuwa mpaka wakati huo hakukuwa kumefanyika uchaguzi wowote wa vyama vingi.

Hivyo kuhamia kwake kulikiongezea uhai, na uchaguzi ulipofanyika alipata kura milioni 1.8 (asilimia 27.8) nyuma ya Rais Benjamin Mkapa aliyepata kura zaidi ya milioni 4.0 (asilimia 61), NCCR Mageuzi ikaibuka na wabunge 19 wakiwamo watatu wa viti maalumu. Profesa Ibrahim Lipumba wa CUF alipata kura 410,000 (asilimia 6.4) huku John Cheyo wa UDP akipata 250,000 (asilimia 4.0)

Kutokana na ushawishi wake, mwaka 1996, Mrema alishiriki uchaguzi mdogo wa Temeke na kuibuka mshindi licha ya kuwa mgombea wa CCM, Abdul Mtiro Cisco aliungwa mkono na vigogo wa chama hicho na Serikali, akiwamo Rais Mkapa.

Hata hivyo, baada ya miaka kadhaa ya neema ikiwamo umoja na mshikamano, vigogo wa chama hicho wakaingia katika mgogoro uliokuwa ukionekana wa kuwania uongozi.

Kutokana na mgogoro huo, zikazaliwa kambi tofauti ambapo moja ilikuwa ikimuunga mkono Mrema nyingine iliyokuwa ikiongozwa na Katibu mkuu, Mabere Marando ilimpinga awali chini kwa chini lakini baadaye mgogoro ukakuwa na kufikia hatua ya wafuasi wake kutwangana makonde vikaoni.

Baadaye Mrema akakubali yaishe mwaka 1999, akaondoka NCCR na kujiunga TLP pamoja na wafuasi wake kama alivyofanya Maalim Seif.

Hilo likawa pigo kubwa kwa chama hicho kwani katika uchaguzi uliofuata mwaka 2000 NCCR ilipata mbunge mmoja tu mkoani Kigoma ambaye hata hivyo hakufika mbali kwani ubunge wake ulitenguliwa na mahakama kabla ya kipindi chake kumalizika.

Chama cha TLP kikapata nguvu kubwa na kuondoka katika kundi la vyama vya siasa visivyo na wabunge kwani ilivuna wabunge wanne huku Mrema akiendelea kupata kura 637,077 za urais zilizokibeba chama hicho kuendelea kupata ruzuku huku NCCR ikiambulia kiduchu.

Kutokana na mazingira hayo, inaonyesha kuwa ikiwa CUF haitakuja na mikakati ya kuepuka migogoro inaweza kufuata njia ile ya NCCR na kuishia kuwa kama iliyo sasa na mbunge mmoja.

Hatima ya CUF, ACT

Profesa Lipumba anasema licha ya kuondoka kwa Maalim Seif chama hicho kitaendelea kupambana na kutunza heshima yake ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wanapata viongozi katika chaguzi mbalimbali.

Hata hivyo, ni ukweli usiopingika kuwa Maalim Seif ni mwanasiasa mwenye kundi kubwa la wafuasi hususani Zanzibar ambako kwa miaka 27 aliyokuwa CUF alionyesha upinzani mkali kwa CCM kwani chama chake kilipata idadi kubwa ya wabunge, wawakilishi na madiwani.

Wakati akitangaza kuihama CUF, Maalim Seif aliwataka wale wanaomuunga mkono ‘kushusha tanga na kupandisha tanga’ akimaanisha waungane naye katika safari ya siasa na kwa jinsi siasa za Zanzibar zilivyo na kwa kile kinachoshuhudiwa sasa kwa wafuasi wa CUF kwenda ACT, bila shaka Lipumba na chama chake watakuwa wamepata pigo kubwa.

Viongozi wote wa juu wa CUF Zanzibar wameamua kuondoka na Maalim Seif na kujiunga ACT Wazalendo.

Kwa upande wa ACT inayoongozwa na Zitto Kabwe inatarajiwa kupata neema kama ile iliyoiangukia NCCR ya Mrema au TLP katika miaka ya mwanzo chini ya mwenyekiti wake huyo.

Kutokana na nguvu kubwa ya Maalim Zanzibar, ni wazi katika uchaguzi mkuu ujao ACT imejiongezea uhakika wa kupata wabunge na wawakilishi kwa nguvu ya Maalim Seif hatua ambayo itakiongezea uimara na pengine kuanza kupata ruzuku kubwa zaidi ya ilivyo sasa.

Hata hivyo, ACT isipokuwa makini na kuitumia vizuri fursa hiyo inaweza kuishia kama TLP iliponufaika kwa muda na Mrema lakini ikaendelea kuporomoka hadi hatua ya sasaambapo haina mbunge wala diwani.