VIDEO: Mikutano ya hadhara na maandamano, Vigogo CCM wamtega Magufuli

Tuesday February 12 2019

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli amepiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano kwa vyama vya siasa, baadhi ya viongozi wa CCM wanaonekana kwenda kinyume na maagizo hayo, wanafanya mikutano hadharani.

Rais Magufuli alipiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano mwaka 2016, akitaka viongozi wa kuchaguliwa tu ndio waendeshe mikutano kwenye maeneo yao husika.

Agizo hilo ambalo amelisisitiza mara kwa mara linaruhusu viongozi wengine wa kisiasa kufanya mikutano ya ndani tu.

Januari 23, alipokutana na viongozi wa dini jijini Dar es Salaam, Magufuli aliulizwa swali na mmoja wa viongozi hao wa dini kuhusu suala hilo na hakusita kuonyesha msimamo wake.

“Uchaguzi unapomalizika katika nchi nyingine zenye demokrasia kubwa, huo uchaguzi umeisha. Wale wabunge waliochaguliwa inabaki kazi yao kwenye majimbo yao na bungeni na kwenye halmashauri”.

CCM wachapa kazi

Advertisement

Lakini hali ni tofauti na agizo la Rais na maelezo ya Kamanda Msangi.

Katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally amefanya mikutano kadhaa nchini na sasa anaendelea na mikutano mkoani Morogoro huku katibu wa itikadi na uenezi, Humphrey Polepole akifanya mikutano hiyo Arusha.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Msowelo wilayani Kilosa mwishoni mwa wiki, Dk Bashiru alimshukia mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu akifananisha jina lake na ugonjwa hatari unaoambukiza ambao alisema dalili zake ni uongo, dharau, rushwa, kiburi, madeko, ubinafsi na unyanyasaji.

Akiwa katika kata hiyo, Dk Bashiru pia alichangisha zaidi ya Sh4 milioni kwa ajili ya ujenzi wa nyumba ya mwasisi wa CCM, Salima Matewele.

Akiongozana na viongozi wa CCM na Serikali wa mkoa katika moja ya mikutano hiyo, Dk Bashiru aliwataka polisi kufanya kazi za kulinda amani na utulivu na si kuivuruga.

Mbali na katibu huyo, Polepole amekuwa katika ziara ya kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi mkoani Arusha, moja ya maeneo ambayo wapinzani wana nguvu.

Akiwa mkoani humo, Polepole alimtaka mkuu wa wilaya ya Karatu, Theresia Mahongo kuhakikisha anatenga Sh30 milioni kwa ajili ya ujenzi wa maabara tatu za sayansi katika shule ya sekondari ya Kansay.

Polepole aliwataka Watanzania kumuombea mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema) apone lakini akamtaka awe makini na matamshi yake.

Mbali na wawili hao, katibu wa siasa na uhusiano wa kimataifa wa CCM, Kanali Ngemela Lubinga ameanza ziara ya siku sita mkoani Njombe akimwakilisha katibu mkuu kwa lengo la kutoa rambirambi katika mauaji ya kikatili ya watato yaliyotokea hivi karibuni.

Kiongozi mwingine wa CCM anayeendelea na ziara ni mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Kheri James ambaye jana alionekana mkoani Simiyu akihutubia mikutano ya hadhara na kukagua miradi ya maendeleo.

Kada mwingine wa CCM na mjumbe wa Halmashauri Kuu, Laila Ngozi ameonekana kwenye mitandao ya jamii akiandamana na wanafunzi wilayani Kongwa Mkoa wa Dodoma.

Hivi karibuni, aliyekuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda alifanya ziara ya kichama mkoani Iringa na kupokelewa na maandamano katika wilaya alizotembelea, ikiwemo wilaya ya Mufindi.

Rais Magufuli ameonyesha msimamo wake huo wa kuzuia mikutano ya hadhara na maandamano katika mikutano yake mbalimbali, lakini wadau wa siasa wamekuwa wakitaka Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa inayotoa uhuru huo viheshimiwe.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu hivi karibuni, msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Ahmed Msangi alisema zuio hilo bado linaendelea na wanaoruhusiwa ni wabunge kwenye maeneo yao.

“Wewe umeshaona mbunge labda wa Kawe amezuiwa? Ndiyo hivyo kwa mikutano ya kisiasa. Hawezi kutoka mbunge wa Nyamagana (Mwanza) akafanya mkutano Kawe, Dar es Salaam, atakuwa anamwingilia mwenye jimbo lake,” alisema Msangi.

Wapinzani walalamika

Hata hivyo viongozi wa vyama vya upinzani hawajakaa kimya kuhusu mikutano hiyo ya CCM.

“Hiyo ni picha halisi ya ukandamizwaji wa demokrasia,” alisema naibu katibu mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alipoulizwa kuhusu suala hilo.

“Waulizwe CCM kwa nini wanaendelea kufanya mikutano na maandamano iliyokatazwa, maana hata mwizi akiiba hutamfuata aliyeibiwa na kumuuliza kwa nini umeibiwa.

“Tukisema ukandamizwaji wa demokrasia, ndio huo maana kama ni kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi, hata sisi tunayo ilani yetu iliyowapitisha wabunge na madiwani. Tumeaminiwa na watu na sisi tuna haki ya kukagua.”

Alipoulizwa kuhusu suala hilo, John Shibuda, mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa alisema wameyasikia malalamiko na wanakusudia kuitisha mkutano wa vyama vya siasa kuyajadili na kutafakari mabadiliko ya sheria ya vyama vya siasa.

Agizo lautesa upinzani

Marufuku hiyo ya mikutano ya hadhara na maandamano imekuwa mwiba kwa wapinzani, ambao kwa nyakati tofauti wamekamatwa kwa kufanya mikutano ya ndani na wengine kufikishwa mahakamani.

Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe amewahi kuzuiwa na polisi mkoani Morogoro na Lindi.

Pia Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alikamatwa Julai 16, 2017 wilayani Nyasa mkoani Ruvuma akiwa na viongozi wa chama hicho Kanda ya Kusini katika mkutano wa ndani.

Desemba 30, 2018, Dk Mashinji na viongozi wengine wa Chadema pia walikamatwa wilayani Hai, Kilimanjaro katika mkutano wa ndani na kuwekwa mahabusu.

Desemba 16, 2018, polisi walivunja mkutano wa ndani wa Chadema uliokuwa ukiongozwa na naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu mjini Mafinga wilayani Mufindi, Iringa.

Advertisement