Mjumbe tume ya Warioba aeleza walichobaini wakurugenzi kusimamia uchaguzi

Muktasari:

Wakati Serikali ikikata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia wakurugenzi kusimamia chaguzi, mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, Ally Saleh amesema Serikali imejiweka pabaya

Dar es Salaam. Wakati Serikali ikikata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga hukumu ya Mahakama Kuu kuwazuia wakurugenzi kusimamia chaguzi, mjumbe wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Ally Saleh amesema Serikali imejiweka pabaya.

Saleh alikuwa miongoni mwa wajumbe 30 walioteuliwa na Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuzunguka nchi nzima kukusanya maoni ya wananchi waliopendekeza muundo wa tume ya uchaguzi. Tume hiyo iliongozwa na  Waziri Mkuu Mstaafu Jaji  Joseph Warioba.

Saleh ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 15 siku chache baada ya Mahakama Kuu kubatilisha kifungu cha 7(1) cha Sheria ya Uchaguzi kinachoipa mamlaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi(Nec) kuwatumia wakurugenzi wa majiji, manispaa na miji kuwa wasimamizi wa uchaguzi.

“Serikali imejiweka pabaya  kama ilivyo katika miaka ya hivi karibuni kuhusu suala hilo (la kukata rufaa), tume ilikwenda kote nchini na wananchi walitaka tume huru, uwakilishi hadi ngazi ya wilaya, kwa hiyo maoni ya Tume ya Warioba yalikuwa ni maono na yatazidi kuonekana baada ya mingi ijayo.”

“Hoja yao wanasema mbona kuna majimbo yaliyosimamiwa na wakurugenzi hao wapinzani walishinda? Lakini ni kwa sababu kulikuwa na mbinde,  watu walipigana, walitishia kuchoma moto ndiyo wakatangaza ushindi,” amesema Saleh.