Mkataba ujenzi viwanda vya ngozi wasainiwa leo

Friday February 8 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Mradi wa ujenzi wa viwanda vya bidhaa za ngozi unatarajiwa kutekelezwa nchini Tanzania ikiwa  ni utekelezaji wa agizo la kuifanya Tanzania ya Viwanda.

Mradi huo unaofahamika kama Karanga Leather Industries Co. Ltd  utatekelezwa katika eneo la Gereza la Karanga lililopo manispaa ya Moshi.

Akizungumza leo Ijumaa Februari 8, 2019 wakati wa utiaji saini mkataba wa ujenzi huo, mkurugenzi mtendaji wa  kampuni ya Karanga, Masudi Omary amesema utekelezaji wa mradi huo utahusisha uboreshaji wa kiwanda cha viatu kilichopo chini ya magereza kwa lengo la kuongeza uzalishaji.

Sanjari na hilo,  mradi utahusisha kuanzishwa kiwanda kipya cha viatu chenye uwezo wa kuzalisha jozi 1.2 milioni kwa mwaka, kiwanda cha soli, kiwanda cha kuchakata ngozi na kiwanda cha kuzalisha bidhaa zitokanazo na ngozi.

Amesema uanzishwaji wa mradi huo ni utekelezaji wa kuanzishwa kwa viwanda vya kutengeneza malighafi.

Kwa mujibu wa Omary mradi huo utatengeneza ajira 3,000 za moja kwa moja na vibarua zaidi ya 4,000.

Advertisement