Mkataba wa kuleta watalii 10,000 kati ya ATCL, TIHG wasainiwa

Tuesday March 12 2019

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),

Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB), Jaji Thomas Mihayo 

By Jackline Masinde, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kampuni ya Ndege ya Tanzania (ATCL) na Kampuni ya Touchroad International Holdings Group (TIHG) ya nchini China wamesaini mkataba wa kuingia kwenye maongezi ya kibiashara ya namna ya kuwasafirisha watalii zaidi ya 10,000 wanaotarajia kuingia nchini Tanzania kwa mwaka 2019.

Awali, TIHG ilisaini mkataba na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) ya kuleta watalii hao 10,000 mwaka jana kwa kutumia ndege zake, hivyo utiaji saini wa mkataba huo na  ATCL  ni mwendelezo wa kuanza kwa utekelezaji wake ambapo kampuni hiyo italeta hapa nchini watalii kutoka China kisha watalii hao watatumia ndege za ATCL kuelekea maeneo mbalimbali ya utalii nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne, Machi 12, 2019, Mwenyekiti wa TTB, Jaji Thomas Mihayo amesema katika kuhakikisha sekta ya utalii inakuwa na mchango mkubwa katika uchumi, imeanza kutekeleza makubaliano ya kuleta watalii 10,000 hapa nchini.

"Hivyo leo tutakuwa na tukio la kusaini mkataba wa kuingia makubaliano ya maongezi ya kibishara kati ya ATCL na  kampuni hii ya China ya namna watakavyofanya biashara ya kusafirisha watalii kuwatoa China na kuwaleta hapa nchini, "amesema.

"Tunatarajia kuanza kupokea watalii  300 kuanzia mwezi Mei mwaka huu, kundi hili la watalii litakuwa la watu maarufu nchini China wakiwamo waandishi wa habari wakubwa, wafanyabiashara wakubwa na wasanii mbalimbali, na tunatarajia kupata watalii 260 kila wiki mpaka hapo watakapokamilika watalii 10,000," amesema.

Kwa upande wake, meneja mauzo na usambazaji wa ATCL, Edward Mkwabi amesema shirika hilo limejipanga kufanya kazi hiyo ya kubeba watalii na kwamba makubaliano yaliyofanyika leo ni ya kuingia kwenye mawasiliano ya namna gani biashara itafanyika.

Naye, Mwenyekiti wa Kampuni ya TIHG, He Liehu amesema kampuni hiyo pia imejipanga vyema kufanya biashara ya kuleta watalii nchini kupitia ndege zake.

Advertisement