Mke wa Netanyahu hatiani kwa ubadhirifu

Jerusalem. Mahakama moja nchini Israel imemtia hatiani mke wa waziri wa nchi hiyo, Benjamin Netanyahu kwa makosa ya ubadhirifu wa fedha za umma kwa chakula, baada ya ‘kukiri kosa ili yaishe’.

Sara alitumia utaratibu wa kukubaliana na mwendesha mashtaka kukiri kosa dogo ili kupata nafuu katika adhabu baada ya kutupa mashtaka mengine

Sara Netanyahu amekutwa na hatia kwa kukumbatia makosa ya mtu mwingine na kuhukumiwa na hakimu Avital Chen kulipa faini na fidia.

Kwa mujibu wa AFP, Sara aliiomba mahakama ikubali ombi la ‘kukiri ili yaishe’ ili impunguzie adhabu ya hukumu ya ubadhirifu wa fedha za umma kwa chakula.

Pamoja na kumaliza kesi hiyo kirahisi, familia hiyo ya waziri mkuu haijawa salama, kwa yeye wenyewe anakabiliwa na uwezekano wa mashtaka ya rushwa, ubadhirifu na kukosa uaminifu.

Baada ya kutiwa hatiani kwa kukumbatia makosa ya mtu mwingine, Sara Netanyahu alihukumiwa kulipa fani ya Shekel 10,000 (Dola za Marekani 2,800) na kurejesha fedha za umma Shekel 45,000.

“makubaliano yaliyofanyika yanaonyesha matendo na kiwango cha uhalifu,” alisema Chen katika hukumu yake.

Sara mwenye umri wa miaka 60 alishtakiwa Juni 2018 kwa ubadhirifu na ukosefu wa uaminifu kwa kununua chakula kwa watoa huduma wakati makazi ya waziri mkuu yana mpishi rasmi wa Serikali.

Mashtaka yaliyofanyiwa marekebisho Jumapili yameachana na mashtaka ya rushwa na kuacha lile la kufanya kazi ya mtu mwingine.

Katika chumba kidogo cha mahakama iliyosheheni waandishi wa habari Sara alikiri kuyafahamu mashtaka yake na wakili wake pamoja na mwendesha mashtaka waliiomba mahakama kukubali maafikiano baina ya pande hizo mbili.

“Kama ilivyo kwa maafikiano mengine yote, kila upande huwa una masuala ambayo huamua kuyapoteza na wakati mwingine yakiwa ni mazito, huu ni wakati muafaka wa kukubali kwa maslahi ya umma kumaliza shauri hili,” alisema Mwendesha mashtaka Erez Padan.

Wakili wa Sara, Yossi Cohen alisema mteja wake tayari alikuwa ameshapata adhabu ya kutosha kupitia vyombo vya habari.

“Miaka minne ya taarifa mbaya dhidi yake ilikuwa ni adhabu tosha isiyo ya kibinadamu...Hakuna mtu mwingine ambaye angehimili hali hiyo. Huyu mama ni wa chuma,” alisema. 

Mashtaka ya awali yalidai kuwa alilipa Dola 100,000 kwa wafanyabiashara kwa ajili ya chakula akidai kuwa hakuwa na mpishi nyumbani kwake.

Watoa huduma za chakula walikuwa Italian Restaurant, Middle Eastern Grill Joint na Sushi House.

Sara pia anashtakiwa na mhudumu wa usafi anayedai kuwa alimtendea isivyo.

Mwaka 2016 mahakama iliamuru amlipe Dola za marekani 47,000 mtunza nyumba wake wa zamani, aliyemtuhumu kwa kumnyanyasa mara kwa mara.

Katika hatua nyingine, Netanyahu anakabiliwa na madai ya rushwa, ubadhirifu na kukosa uaminifu.

Kutokana na tuhuma hizo, inasemekana Netanyahu anataka kubadili sheria ili aweze kupata ulinzi kisheria. Hata hivyo alishindwa kuunda Serikali ya mseto kutokana na Uchaguzi Mkuu wa Aprili, hivyo bunge limevunjwa akisubiri uchaguzi mwingine Septemba.