Moto wateketeza ghala la tume ya uchaguzi DRC

Muktasari:

Siku 10 kabla ya kufanyika Uchaguzi Mkuu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), vifaa vyote vya uchaguzi vilivyokuwa vimehifadhiwa kwenye ghala mjini Kinshasa vimetetea kwa moto hali inayozusha wasiwasi kuhusu kufanyika kwa uchaguzi huo Desemba 23, 2018

Kinshasa. Moja ya ghala kubwa za Tume Huru ya Uchaguzi ya Jamhuri ya Kidemokasia ya Congo (CENI) limeteketea kwa moto, ikiwa  bado siku 10 ufanyike Uchaguzi Mkuu nchini humo.

Taarifa zilizothibitishwa na vyanzo mbalimbali vya habari zinaeleza kuwa ghala hilo lililoteketea liko mjini Kinshasa.

Moto huo uliozuka katika ghala hilo jana usiku Desemba 12, 2018 umesababisha hasara kubwa. Vifaa viliokuwa katika ghala hilo karibu vyote vimeteketea kwa moto.

Tukio hilo linatokea ikiwa zimesalia siku kumi kabla ya Uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika Desemba 23, 2018

"Moto ulizuka karibu saa nane usiku saa za Kinshasa katika moja ya ghala kuu ambapo kulikuwa kumehifadhiwa vifaa vya uchaguzi katika mji wa Kinshasa," amesema mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (CENI), Corneille Nangaa.