Mshahara wa Lissu wawaibua Chadema, wamjibu Ndugai

Muktasari:

  • Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakijawahi kushuhudia chuki dhidi ya wabunge kama inayofanywa kwa Tundu Lissu

Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakijawahi kushuhudia chuki dhidi ya wabunge kama inayofanywa kwa Tundu Lissu.

Kimetoa kauli hiyo kupitia taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Februari 7, 2019 na Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho, John Mrema ikiwa ni saa chache tangu mbunge wa Geita (CCM), Joseph Kasheku ‘Msukuma’ kutaka mshahara wa Lissu usitishwe kwa madai ameshapona na anachofanya sasa ni kuitukana nchi katika ziara zake ughaibuni.

Kauli ya Musukuma iliungwa mkono na Spika Job Ndugai akisema jambo hilo lina ukweli kwa maelezo kuwa Lissu ambaye ni mbunge wa Singida Mashariki hayupo bungeni, jimboni na hana taarifa za daktari.

Mrema amesema Chadema imesikitishwa na kadhia hiyo dhidi ya Lissu aliyeshambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 Septemba 7, 2017.

“Tunamkumbusha Spika wa Bunge wapo wabunge wengi kwenye historia ya Bunge letu ambao wamewahi na wengine wapo kwenye matibabu, haijawahi kutokea tukashuhudia kiwango kikubwa cha chuki dhidi yao kama ambavyo tunashuhudia kwa Lissu ambaye jaribio la mauaji lilishindikana kwa miujiza ya Mungu,” amesema Mrema na kuongeza:

“Chadema tunasikitishwa na kauli hizi kwani ni uthibitisho wa wazi kuwa Bunge lilipokataa kulipia matibabu ya Lissu walikuwa wana nia mbaya dhidi ya maisha yake na walipoona Watanzania wameendelea kulipia matibabu yake imewaumiza.

“Chadema tunamtaka Spika wa Bunge asimamie sheria na kanuni za Bunge na ajue kuwa wabunge wana haki ambazo zipo kwa mujibu wa sheria na hawafanyi kazi zao kwa kutegemea fadhila.  

“Tunawaomba wanachama wetu wamuombee Spika na wabunge ili waachane na 'roho za chuki' dhidi ya Lissu ambaye Mungu alimuokoa baada ya kupigwa risasi 16 zilizoingia ndani ya mwili wake.”

 

                    >>Sakata la upelelezi kesi ya Lissu laibuka bungeni