Sakata la upelelezi kesi ya Lissu laibuka bungeni

Muktasari:

Sakata la upelelezi wa kesi ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu aliyepigwa risasi Septemba 7 mwaka 2017 limeibua majibizano kati ya Mbunge wa Rombo (Chadema) Joseph Selasini na Spika wa Bunge, Job Ndugai.


Dodoma. Sakata la upelelezi wa kesi ya mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) Tundu Lissu  limeibua majibizano kati ya mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini na Spika Job Ndugai.

Majibizano hayo yameibuka wakati Selasini akichangia taarifa ya kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa bungeni leo Februari 7 mwaka 2019.

Amesema alizoea kuwaona Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Lissu na mbunge wa Tarime Mjini (Chadema), Esther Matiko wanavyoketi ndani ukumbi wa bunge lakini sasa hawapo inamuuma. Mbowe na Matiko wapo mahabusu baada ya kufutiwa dhamana kutokana na kutoonekana mahakamani.

“Nichukue nafasi hii kuwapa pole wenzangu na kuwaombea mitihani inayowakabili waipokee na mwenyezi Mungu awajalie tuweze kuwa pamoja siku moja na ninajua itakuwa hivyo,” amesema.

Selasini amesema kuwa  utawala bora ni jambo la msingi na kutolea mfano kauli ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola juzi bungeni kuhusu upelelezi wa kesi ya Lissu.

Amesema  sheria ya  Upelelezi ya Masuala ya Kijinai (The Mutual  assistance  in  criminal matters) ambayo inawezesha mtu kuchukuliwa  maelezo popote.

Huku akihoji sababu za Lissu kutofuatwa Nairobi na Ubelgiji alilokwenda kutibiwa baada ya kushambuliwa na risasi zaidi ya 30, Septemba 7, 2017, Selasini ametoa  wito kwa viongozi na wabunge kufuata sheria ambazo wamezitunga wenyewe bungeni.

Hata hivyo, Spika wa Bunge Job Ndugai alimkatisha na kubainisha kuwa si sahihi kumlaumu Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola.

Ndugai alimtolea mfano dereva wa Lissu kwamba anaweza kurejea nchini kutoa ushahidi wa kesi hiyo ya kupigwa risasi.

Katika majibu yake Selasini amesema wote wawili (Lissu na dereva wake) wako kwenye matibabu na kwamba wanaoweza kutolea maelezo ya matibabu yao ni madaktari wanaowatibu.

“lakini hii sheria Wizara ya Mambo ya Ndani inaweza kuitumia hata huyu dereva popote alipo akahojiwa,” amesema Selasini.

Kauli hiyo iliibua swali jingine kutoka kwa Ndugai akitaka kufahamu iwapo madaktari walishaandika chochote kuleta nchini.

Hata hivyo, Selasini alijibu kuwa ili kuondoa sintofahamu na kelele zinazopigwa mitaani  ni vyema sheria hiyo ikafuatwa.

Hata baada ya jibu hilo, Ndugai bado alimweleza Selasini kuwa madaktari wanapaswa kuandika taarifa ili ije nchini.