VIDEO: Ndugai ampa tano Musukuma kuondoa mshahara wa Lissu

Muktasari:

Mbunge wa Geita (CCM),  Joseph Kasheku 'Musukuma' amehoji ni lini Bunge litasitisha mshahara wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),  Tundu Lissu aliyedai kuwa amepona na sasa anaitukana Serikali


Dodoma. Mbunge wa Geita (CCM),  Joseph Kasheku 'Musukuma' amehoji ni lini Bunge litasitisha mshahara wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema),  Tundu Lissu aliyedai kuwa amepona na sasa anaitukana Serikali.

Musukuma ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 7, 2019 bungeni jijini Dodoma baada ya kuomba mwongozo wa Spika.

"Lissu anazunguka huku anasemekana anaumwa, ni lini Bunge litasitisha mshahara wake kwa sababu ameshapona na ameendelea kuzunguka huko na huko akitukana Bunge na Serikali," amehoji Musukuma.

Akijibu mwongozo huo, Spika Job Ndugai amesema suala hilo linahitaji kuangaliwa kwa upekee.

"Jimboni hayupo, bungeni hayupo, nchini hayupo, hospitali hayupo na mimi sina taarifa yoyote wala ya daktari. Hoja yako ina msingi iko haja ya kusimamisha mishahara wake," amesema Ndugai.

Amesema atayafanyia kazi mambo yaliyo ndani ya uwezo wake.