Collymore wa Safaricom Kenya afariki dunia

Monday July 1 2019

 

By Mwandishi wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Aliyekuwa ofisa mtendaji mkuu wa kampuni ya Safaricom nchini Kenya, Bob Collymore amefariki dunia leo asubuhi, Julai Mosi, 2019.

Taarifa iliyotolewa na mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa Safaricom, Nicholas Nganga imesema Collymore alikuwa anasumbuliwa na saratani kwa muda mrefu.

“Oktoba 2017 alienda Uingereza kwa matibabu na akarejea Julai 2018 kuendelea na majukumu yake huku akihudhuria hospitali kila ilipobidi. Mara ya mwisho alikuwa anatibiwa katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan hapa Nairobi kabla hali yake haijawa mbaya zaidi,” amesema Nganga.

Raia huyo wa Uingereza ambaye hivi karibuni aliteuliwa kuwa mjumbe wa bodi ya taasisi ya saratani nchini Kenya, ameacha mke, Wambui Kamiru, na watoto wanne.

Kifo cha Collymore (61), kimetokea mwezi mmoja kabla hajastaafu kwani alipanga kuachia wadhifa huo Agosti mwaka huu.

Katika kipindi cha uongozi wake katika kampuni hiyo kubwa ya mawasiliano Afrika Mashariki, Safaricom imeweza kuisogeza mbele huduma ya M-Pesa iliyozinduliwa mwaka 2007, hivyo kuleta mageuzi katika sekta ya fedha Afrika.

Advertisement

Wakati Afrika ikisifika duniani kwa ubunifu huo, Collymore ni miongoni mwa watu muhimu katika maendeleo hayo ambayo sasa yanawanufaisha mamilioni ya wananchi huku ikirahisisha huduma za benki za biashara pia.

Tangu alipoanza kuiongoza kampuni hiyo mwaka 2010, Collymore amaeifanya Safaricom kuwa kampuni kubwa nchini Kenya inakohudumia wateja wawili katika kila watu watano wanaotumia simu ya mkononi.

Advertisement