Mtoto adaiwa kumuua kwa panga mwenzake wa mwaka mmoja

Wednesday July 24 2019

 

By Hamida Shariff, Mwananchi [email protected]

Morogoro. Polisi mkoa wa Morogoro nchini Tanzania linawashikilia baba na mtoto wake wa miaka nane kwa tuhuma za kumuua mtoto wa jirani yao mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi saba kwa kumkata mapanga kichwani.

Tukio hilo lilitokea Jumapili iliyopita Julai 21, 2019 saa 8 mchana katika kijiji cha Hembeti wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ambapo mwili wa mtoto huyo, Greyson Valentino ulikutwa umefichwa kwenye shamba la watuhumiwa ukiwa na majeraha.

Akizungumzia tukio hilo leo Jumatano Julai 24, 2019, Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro,  Wilbroad Mutafungwa amewataja watumiwa ni Said Stephen ambaye ni baba na mwanae wa kike (jina linahifadhiwa) ambaye ni mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Mpapa wilaya ya Mvomero

Kamanda huyo amesema siku ya tukio baba wa marehemu, Simon Shedrack akiwa kanisani alipata taarifa kuwa mtoto wake amepotea na hivyo aliamua kurudi nyumbani kuanza kumtafuta kwa kushirikiana na majirani zake.

Amesema katika harakati za kumtafuta walipita kwenye shamba la mtuhumiwa na kuukuta mwili wa mtoto wake ukiwa na majeraha kichwani.

Kamanda huyo amesema baada baba wa marehemu kwenda nyumbani kwa mtuhumiwa ili kuhoji kwa nini mwili wa mtoto wake umekutwa kwenye shamba hilo ndipo mdogo wa mtuhumiwa (jina linahifadhiwa) alipoeleza alimuona dada yake akimuua mtoto huyo kwa kutumia panga kisha kumuweka shamba.

Advertisement

Mutafungwa amesema baada ya tukio hilo wananchi walimkamata mtoto huyo aliyetajwa kuhusika na mauaji hayo na kumfikisha katika kituo cha polisi Dakawa akiwa na panga alilotumia kufanyia mauaji hayo.

Amesema baada ya kuhojiwa alikiri kufanya tukio hilo la mauaji.

Mutafungwa amesema polisi waliendelea na msako na kufanikiwa kumkamata baba wa mtoto huyo (Stephen) na kumuunganisha katika tuhuma hizo za mauaji kwani baada ya tukio hilo alikimbia na hata alipopewa taarifa za tukio hilo hakutoa ushirikiano kwa polisi wala familia ya marehemu.

Amesema pamoja na kuwashikilia watuhumiwa hao ambao ni baba na mtoto wake bado polisi wanaendelea na uchunguzi zaidi kuhusiana na tukio hilo na baada ya kukamilika hatua za kuwafikisha mahakamani zitafuata.

Hata hivyo, amesema mwili wa marehemu umeshafanyiwa uchunguzi wa kidaktari na tayari wazazi wameshakabidhiwa kwa ajili ya taratibu za mazishi.

Advertisement