VIDEO: Mtoto wa Ruge awaliza watu akimuombea msamaha baba yake

Sunday March 3 2019

By Waandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jana ilikuwa siku iliyogubikwa na wingu la majonzi wakati wakazi wa jiji la Dar es Salaam walipojitokeza kuaga mwili wa aliyekuwa mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group, Ruge Mutahaba.

Katika viwanja vya Karimjee mavazi ya rangi nyeusi yalitawala na wengi walikuwa wakitokwa machozi, na hata ambaye hakutoa machozi alishika tama.

Na wengi walibubujikwa na machozi wakati wa hotuba fupi na yenye hisia kali iliyotolewa na mwanae Ruge.

Mwachi, ambaye ni mtoto wa kwanza wa Ruge, aliwatoa machozi karibu watu wote waliohudhuria maziko hayo jana, baada ya kusema anamuombea msamaha baba yake kwa wale aliowakosea enzi za uhai wake.

Baadhi walionekana kuinama wakifuta machozi wakati kijana huyo akiendelea kusoma wasifu wa baba yake huku naye akibubujikwa na machozi.

“Ninamuombea msamaha baba yangu kwa wale wote aliowakosea enzi za uhai wake. Nasi tunawasamehe wote waliomkosea baba,” alisema Mwachi ambaye ni mmoja kati ya watoto watano wa Ruge.

Advertisement

Alisema baba yake alikuwa mtu aliyejitoa kwa maisha ya wengine mpaka familia ilifikia wakati inaona watu wa nje wanamfaidi kuliko wao.

Mwachi, ambaye muda wote alikuwa akijizuia kutoa machozi, alisema angalau wakati baba yake anaumwa ndipo walipopata muda mwingi wa kukaa naye kama familia.

“Alitenga muda mwingi kusaidia kwa kuzingatia misingi ya utu, alipambana kwa hali zote kufanikisha mambo mengi katika jamii,” alisema huku sauti yake ikitetemeka akionekana kujizuia kulia.

Alisema jamii inachoweza kufanya ni kuchukua jukumu la kusaidia japo Watanzania wawili, watafanikisha ndoto za wengi.

Katika maziko hayo yaliyoongozwa na Rais John Magufuli, wanamuziki Nandy na Khadija walishindwa kuimba na kuondolewa jukwaani.

Nandy alipangwa kuimba wimbo “Nikumbushe Wema Wako” ambao ilidaiwa kuwa marehemu alikuwa akipenda kuusikiliza.

Mwanamuziki mwingine, Barnaba ambaye anamtaja Ruge kama baba yake mlezi, naye alishindwa kuendelea kuzungumza alipopewa nafasi hiyo na hivyo kutolewa nje na watu wa huduma ya kwanza.

Awali mkurugenzi wa Clouds Media, Joseph Kusaga, ambaye ni rafiki yake mkubwa na mshirika, alisema Ruge aliwahi kumwambia kuwa wakati wa kifo chake waombolezaji washerehekee maisha yake na kumshukuru Mungu.

“Alisema nikichomoka hakikisha mnakula raha, ikiwezekana na hata hizi nyimbo za huzuni achana nazo,” alisema Kusaga.

“Tunasherehekea maisha ya mtoto wa Kitanzania ambaye angeweza kubaki Ulaya alikoenda kusoma, lakini wazazi wake walimwambia kama ni kitu unachotaka pambana nacho,” alisema Kusaga.

Naye Waziri wa Mazingira, January Makamba alisema utu wa Ruge unapimwa katika yale aliyoacha duniani.

Amesema wengine wanaweza kuwa na vyeo, pesa na mali nyingi lakini wasipate heshima kubwa kama aliyoipata Ruge.

“Nimelia peke yangu, nimelia kwa sababu sijalipa deni kubwa la heshima uliyonipa. Ulinipa upendo wa dhati kabisa na tulipanga vitu fulani hivi lakini umeondoka kabla hatujafanya, nimechanganyikiwa,” alisema January.

Kiongozi huyo aliyemaliza hotuba yake kwa kuimba wimbo wa “Hello Hello Tanzania” alisema Ruge alipenda na aliagiza siku ya kuondoka duniani watu waimbe.

“Ndoto na fursa ndio maneno mawili ambayo Ruge aliyapenda. Msiba huu umetuunganisha Watanzania bila kujali vyama na msiba huo umetoa fursa ya ndoto yake kudumu,” alisema.

Alimtaka kila mmoja kujiuliza bango lake limeandikwaje na litasomekaje wakati akifa.

“Leo tunatua bango la Ruge likisomeka vizuri. Jiulize leo ukiondoka bango lako linasomekaje? Sisi kuja kwetu hapa tumekuja kumvisha taji la heshima. Wengine tunaweza kuwa na madaraka ya vyeo, pesa nyingi na mali nyingi lakini tusipate heshima hii.”

Tofauti na misiba mingine ya watu maarufu ambao si wanasiasa, shughuli ya jana ilihudhuriwa na viongozi wakubwa wa Serikali wakiongozwa na Rais Magufuli, ambaye katika salamu zake wakati taarifa za kifo zilipotolewa, alimuelezea Ruge kama “mtoto wake”.

Mwili wa Ruge uliwasili Karimjee saa 4:00 asubuhi na kupokelewa na mamia ya waombolezaji wakiwemo wafanyakazi wa Clouds Media Group, wasanii, waandishi wa habari, wanasiasa na wafanyabiashara.

Wasafi washiriki maziko

Jana pia alitokea mwanamuziki nyota wa miondoko ya Bongo Fleva, Diamond Platnumz, ambaye alikuwa kimya tangu kutolewa kwa taarifa za kifo cha Ruge.

Alifika kushiriki kuaga mwili kwa wakati tofauti na msanii mwingine kutoka kampuni ya Wasafi, Harmonise na meneja wao, Babu Tale.

Aliyeanza kuingia ni Babu Tale na akafuata Harmonize kabla ya Diamond kuwasili akiwa na mama wa msanii wa filamu, Sanura.

Uwepo wao katika viwanja hivyo ulikuwa kivutio kutokana na uhasimu wa kibiashara uliopo baina ya Clouds Media Group na Wasafi Media, ambayo pia imeanzisha vituo vya redio na televisheni.

Mbali na Babu Tale, Diamond na Harmonize, Rommy Jones ambaye ni Dj na kaka wa Diamond Platnumz, walikuwa miongoni mwa waombolezaji waliofika jana.

Rommy Jones pia ni mume wa mzazi mwenza wa Ruge Mutahaba anayefahamika kwa jina moja la Kay.

Mbali na Babu Tale na Rommy Jones, mamia ya waombolezaji walijitokeza katika viwanja hivyo kumuaga Ruge ambaye pia ni mwanzilishi wa semina za Fursa na tuzo za Malkia wa Nguvu.

Wasanii wengine waliofika ni Hamisa Mobeto, Rich Mavoko, Ali Kiba na ndugu yake Abdu Kiba, Batuli, Shilole, Dogo Janja, Madee na wanamuziki wa THT.

Mwili wa Ruge utasafirishwa kwenda kwao Kagera leo asubuhi na kuagwa kwenye viwanja vya Gymkhana mjini Bukoba kabla ya kupelekwa Kijiji cha Kiziru kwa maziko ambayo yatafanyika kesho.

Ruge alifariki dunia Februari 26 2019 nchini Afrika ya Kusini alikokuwa akipatiwa matibabu.

Alikwenda Afrika Kusini takriban miezi minne iliyopita baada ya kusumbuliwa na figo.

Awali alikwenda kutibiwa India na kurudi akiwa na hali nzuri, lakini baada ya kukaa Dar es Salaam kwa muda, hali ilibadilika na kulazimika kwenda Afrika Kusini.

Ruge ni mmoja wa waasisi wa Clouds Media Group, kwa mujibu wa Joseph Kusaga, ambaye alisema walikutana naye zaidi ya miaka 20 iliyopita na kuamua kuanza biashara naye.

Imeandikwa na Asna Kaniki, Rhobi Chacha, Tumaini Msowoya, Khadija Shomari, Hellen Hartley.

Advertisement