Mtwara waomba kivuko cha kudumu mpaka wa Kilambo

Muktasari:

  • Wajumbe wa kikao cha bodi ya barabara Mtwara wameiomba Serikali ya Tanzania kujenga daraja la kudumu katika mto Ruvuma unaounganisha nchi ya Tanzania na Msumbiji.

Mtwara. Kutokana na mpaka wa Kilambo katika mto Ruvuma mkoani  Mtwara unaounganisha nchi za Tanzania na Msumbiji kutumiwa na watu wengi wanaotembelea nchi hizo, wajumbe wa bodi ya barabara mkoani Mtwara wameiomba serikali kujenga daraja la kudumu litakalounganisha nchi hizo kurahisisha usafiri.

Pia, daraja hilo wakati wa kiangazi kivuko hushindwa kufanya kazi kutokana na maji kupungua katika mto Ruvuma.

Akizungumza Jumanne ya Julai 16,2019 katika kikao cha bodi ya barabara mkoa wa Mtwara, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora, George Mkuchika a lisema baada ya kuridhika na wingi wa magari yanayoenda Msumbiji hadi Afrika Kusini wanaiomba serikali kujenga daraja la kudumu Kilambo.

Katika kikao cha mwaka 2018 wajumbe hao waliadhimia kuomba maombi ya daraja kuwekwa kwenye ilani ya uchaguzi lakini hakukuwa na majibu.

“Hili la ilani ya uchaguzi itatekelezwa mwakani Oktoba na utekelezaji wake ni baada ya uchaguzi kama itawepo, sisi tunaomba daraja leo, ilani inaomba daraja kuanzia mwaka 2020-2025,”amesema Mkuchika

Mwenyekiti wa kikao hicho ambaye ni mkuu wa mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa amesema pamoja na kuomba jambo hilo kuingia kwenye ilani ya chama cha Mapinduzi hawapotezi nafasi kuomba serikali.

“Naomba sekretarieti tulipokee na sisi kama serikali kweli tutatuma maombi kwa waziri wa uchukuzi na maombi yake tuombe yawe chanya,” amesema Byakanwa

Mbunge wa Mtwara vijiji (CCM), Hawa Ghasia alisema daraja hilo ni muhimu kwa mkoa wa Mtwara na nchi ya Msumbuji na kwamba kutoka Mtwara mjini kufika lilipo ni kilomita 40.

“Kutoka Mtwara makau makuu hadi Mtambaswala(lilipo daraja linguine la kudumu) ni kilometa zaidi ya 300,lakini mtu akitoka Dar es Salaam akishafika Mnazi mmoja kuja Mtwara inamuhitaji kama kilometa 150 anakuwa ameshafika lakini Mtambaswala ni zaidi ya kilometa 300,”alisema Ghasia