Muswada kupelekwa Mahakama ya Rufani

Muktasari:

  • Uamuzi wa Mahakama Kuu wadaiwa una kasoro za kisheria

Dar es Salaam. Baada ya Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi ya kikatiba ya kupinga muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018, sasa walalamikaji wameamua kuupeleka Mahakama ya Rufani kuhoji uhalali wa uamuzi huo.

Awali, shauri hilo lilifunguliwa Mahakama Kuu Masjala Kuu na viongozi watatu wa vyama vya siasa vya upinzani; Zitto Kabwe, Joran Bashange na Salim Bimani dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG). Zitto, kiongozi wa Chama cha ACT- Wazalendo; Bashange, kaimu katibu mkuu wa Chama cha Wanacnhi (CUF) Bara na Bimani, mkurugenzi wa habari CUF wote kutoka kambi ya Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad walikuwa wakiwakilisha muungano wa vyama 10 vya upinzani.

Katika shauri hilo kwanza walikuwa wakipinga kifungu cha 8 (3) cha Sheria ya Utekelezaji wa Haki za Msingi kinachozuia muswada kupingwa mahakamani, wakiiomba Mahakama itamke kuwa kinakiuka Katiba. Pili, walikuwa wakipinga muswada huo wakidai unakiuka haki za kikatiba za kisiasa kwani unazifanya shughuli mbalimbali za kisiasa kuwa jinai na unampa mamlaka makubwa Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia mambo ya ndani ya vyama hivyo ikiwamo ya uongozi.

Hata hivyo, Mahakama Kuu katika uamuzi wake uliotolewa Jumatatu hiyo na Jaji Dk Benhajj Masoud, alitupilia mbali shauri hilo baada ya kukubaliana na pingamizi la awali lililowekwa na AG, kupinga usikilizwaji wa shauri hilo.

Katika uamuzi wake huo, Jaji Masoud alikubaliana na hoja mbili za pingamizi la AG kuwa shauri hilo liko mahakamani isivyo halali kwa kuchanganya maombi mawili tofauti katika shauri moja na kukiuka sheria inayoelekeza kutumia njia zilizoko kutafuta haki kabla ya kwenda mahakamani.

Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, Zitto na mmoja wa mawakili wao, Daimu Halfani walisema wameamua kwenda Mahakama ya Rufani kupeleka maombi ya mapitio kuiomba mahakama hiyo ipitie uamuzi huo wa Mahakama Kuu.

Halfani alisema katika uamuzi huo kuna suala la tafsiri ya kisheria ambayo haipaswi kuachwa ipite hivyohivyo, kwani una kasoro za kisheria ambazo zitakuwa na athari katika uamuzi wa mashauri mbalimbali yatakayofuatia.

“Tunakwenda (Mahakama ya Rufani) by way of revisio (kwa njia ya mapitio) ili waweze ku-correct (kusahihisha) hizo irregularities (dosari) huko mbele,” alisema Halfani.

Alisema kwa sasa wanafuatilia kupata nakala ya mwenendo na uamuzi wa shauri hilo ili waweze kuwasilisha rasmi maombi yao ya marejeo.