Muswada wa vijana wa miaka 15 kupewa huduma za Ukimwi waja

Muktasari:

Wizara ya Afya imesema inatarajia kupeleka muswada wa sheria bungeni wa kuruhusu vijana mpaka miaka 15 kupata huduma za Ukimwi na kwamba ikiwa utapitishwa na kuwa sheria utasaidia vijana kupata huduma hizo kwa haraka bila ridhaa ya mzazi au mlezi kama ilivyo sasa.


Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania inatarajia kupeleka bungeni Muswada wa Sheria wa kushusha umri wa kuridhia vijana kupata huduma za Ukimwi kutoka miaka 18 hadi 15 ili kupunguza wimbi la maambukizi mapya ya virusi hususani kwa vijana.

Hatua hiyo imekuja baada ya Tume ya Taifa ya Kuthibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS)), kubainisha kuwa kwa siku zaidi ya watu 200 hupata maambukizi mapya ya VVU, huku kati yao vijana 80 wenye umri wa miaka 15 hadi 24.

Hayo yamebainishwa hivi karibuni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk Faustine Ndugulile wakati akizindua shughuli  ya upandaji wa mlima Kilimanjaro (Kilimanjaro Challenge 2019) na kuendesha harambee ya kuchangisha fedha kwa mwaka 2019 kwa ajili ya afua za Ukimwi nchini.

“Serikali tumeanza kuliona hilo na kuchukua hatua, takwimu zinaonesha kuanzia  wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 19, asilimia 27 ni wajawazito au wana watoto, kwa hali hii ya maambukizi tumeamua kupeleka muswada bungeni kushusha umri wa ridhaa hadi miaka 15. Ili sasa iweze kuruhusu kijana kuweza kupata huduma, kwa sababu kwa sasa inabidi apate ridhaa ya mzazi au mlezi,” amesema Dk Ndugulile.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tacaids, Dk Leonard Maboko alisema muswada huo ukipitishwa na kuwa sheria utasaidia vijana kupata huduma za Ukimwi kwa haraka bila ridhaa ya mzazi au mlezi kama ilivyo sasa hali itakayopunguza maambukizi.

Alisema hadi sasa tayari wamekusanya zaidi ya Sh1.5 bilioni sawa na asilimia 67 ya lengo la kampeni hiyo ya mwaka 2019 ambayo kampeni hiyo inatimiza miaka 17 tangu kuanzishwa kwake na asasi na taasisi mbalimbali 50 zinazoshughulikia masuala ya Ukimwi zimenufaika.

Kutokana na tatizo hilo Makamu wa rais miradi endelevu wa kampuni ya AngloGold Ashanti, GGM, Simon Shayo alisema kwa mwaka huu katika kampeni hiyo ya kuchangia afua za Ukimwi wamelenga kukusanya Sh2 bilioni.