Mvua kubwa yaivuruga Dar

Watumiaji wa vyombo vya usafiri na watembea kwa miguu wakipita kwa shida katika Barabara ya Kijiwe Samli jana kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam. Picha na Omar Fungo

Muktasari:

Chacha alisema tatizo la Mto Msimbazi kufurika linatokana na mchanga kuziba njia za maji, lakini akailaumu Serikali kuwakataza wananchi kuuchimba.

Dar/Unguja. Mvua zinazoendelea kunyesha sehemu mbalimbali nchini, zimevuruga miundombinu jijini Dar es Salaam na kusababisha adha ya usafiri, ikiwa ni pamoja na barabara muhimu kufungwa kwa muda.

Kufungwa kwa Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani kuliathiri wakazi wanaotumia njia hiyo kuingia katikati ya jiji na kwa kutumia magari binafsi au mabasi yaendayo haraka (Udart).

Mbali na barabara hiyo kufungwa, maeneo kadhaa yaliathiriwa na maji yaliyotuama barabarani, hali iliyotatiza shughuli za kiuchumi na kijamii zisifanyike ipasavyo.

“Mwaka juzi hali ilikuwa kama hii, mwaka jana tuliambiwa kuwa kuna mradi wa upanuzi wa Mto Msimbazi, lakini hadi leo hakuna kilichofanyika,” alisema Awadh Mahfudhi aliyekuwa akitembea kutoka Magomeni Mapipa kwenda Fire

Mwenda kwa miguu mwingine, Ramadhani Said aliyekuwa barabara hiyo, alisema anashangazwa hali kuwa mbaya zaidi ya miaka iliyopita.

“Naamini (Serikali) hawajaamua, wakiamua hapa tatizo lina ufumbuzi,” alisema.

Lakini hali hiyo ilikuwa neema kwa mwendesha guta, Boniface Chacha aliyesema ametumia chombo hicho chenye matairi matatu ya baiskeli kusafirisha abiria eneo hilo tangu saa 11:00 alfajiri baada ya maji kujaa kwa kuwa magari na bajaji zilishindwa kuvuka.

“Nambeba abiria kutoka ng’ambo hii ya Fire kwenda Magomeni kwa Sh500 kwa guta na wale wa bajaji wanafanya hivyo, wanaopanda pikipiki hulipa Sh1,000 kwa kipande hiki tu,” alisema.

“Wsiokuwa na fedha wanateseka na kuhatarisha maisha kupita kwenye maji haya yanayokimbia kwa kasi.”

Alisema licha ya kumfungulia fursa ya biashara, hali hiyo haiondoi ukweli kuwa wananchi wanapata adhabu kila mvua zinaponyesha na kusababisha barabara hiyo ifungwe.

Chacha alisema tatizo la Mto Msimbazi kufurika linatokana na mchanga kuziba njia za maji, lakini akailaumu Serikali kuwakataza wananchi kuuchimba.

Mvua zaidi zaja Dar

Wakati maeneo mbalimbali jijini hapa yakiathiriwa na mvua hizo zilizonyesha kwa takriban siku tatu, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), imetoa angalizo la uwepo wa mvua kubwa zitakazoambatana na upepo mkali na mawimbi.

Mikoa iliyotajwa kukumbwa na hali hiyo ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Lindi, Mtwara, visiwa vya Unguja na Pemba.

TMA imeeleza kuwa hali hiyo itadumu kwa siku nne kuanzia leo.

Polisi wafungua barabara

Barabara hiyo ilifunguliwa saa 7:08 mchana na mkuu wa Usalama Barabarani Kanda Maalumu ya Dar es Salaam (ZTO), Marson Mwakyoma alisema waliifungua baada ya kujiridhisha kuwa kila kitu kiko sawa na magari yanaweza kupita.

“Kwa kawaida huwa tunapima kupungua maji na wingi wa tope kabla hatujafungua barabara na kujiridhisha kuwa gari zinaweza kupita,” alisema Mwakyoma.

Mvua hizo pia zilisababisha athari kwa zaidi ya nyumba 141 za Wilaya ya Mjini Unguja, Zanzibar katika Shehia ya Mwanakwerekwe, Tomondo, Ziwa Maboga, Ziwatuwe, Pangawe na Kinuni.

Mkuu wa Wilaya ya Mjini Unguja, Marina Joel Thomas alisema wananchi wanapaswa kuwa makini kwa kuhama maeneo hatarishi.

Hata hivyo, naibu mkurugenzi wa Kamisheni ya Kukabiliana na Maafa Zanzibar, Muhidini Ali Muhidini alisema wananchi wamehamasika kuhama.