Mvua yawasotesha njiani abiria kwa saa nne Arusha, Kilimanjaro

Muktasari:

Mvua kubwa zimesababisha magari kukwama kwa zaidi ya saa nne na kusababisha abiria kushindwa kufika katika maeneo mbalimbali kuendelea na shughuli zao katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro

Moshi. Mawasiliano kwa baadhi ya wakazi wa Moshi na Arusha yalikatika kwa muda baada ya mto Biriri kufurika maji na kutopitika kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha maeneo hayo.

Hali hiyo imesababisha usumbufu kwa wasafiri waliokuwa wakitokea Arusha kuelekea Kilimanjaro, Tanga na Dar es Salaam pamoja na waliokuwa wakitokea mkoa wa Kilimanjaro kuelekea Arusha.

Akizungumza leo Jumanne Aprili 30, ofisa tarafa ya Masama wilaya ya Hai, Nsajigwa Ndagile  amesema magari yalianza kukwama kuanzia leo alfajiri hadi saa 4:00 asubuhi baada ya maji kupungua.

"Mvua zilizonyesha usiku hadi leo asubuhi zimesababisha mafuriko na  daraja kujaa maji. Magari  yalizuiwa na polisi walilazimika kukaa eneo hili kudhibiti.”

“Tunashukuru maji yamepungua na kwa sasa magari yameanza kuruhusiwa na foleni iliyokuwa kubwa sana sasa imeanza kupungua,” amesema.

Mwenyekiti wa chama cha wasafirishaji mikoa ya Kilimanjaro na Arusha (Akiboa), Hussein Mrindoko, amesema mawasiliano ya barabara hiyo katika eneo la Msomali yalikatika saa 12:00 asubuhi.

"Mvua zilianza kunyesha usiku (wa kuamkia leo) saa 7:00 na kusababisha mto Biriri kufurika maji na kupita juu ya barabara. Kuna hali ngumu. Foleni ni kubwa sana," amesema Mrindoko.

Katibu Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania (Taboa), Enea Mrutu amesema magari yalizuiwa kuendelea na safari pia katika eneo la King'ori, KIA na eneo la Msomali kutokana na mafuriko hayo.

Mmiliki wa mabasi ya Capricorn, George Mberesero amesema hadi muda huo magari bado yalikuwa hayajaruhusiwa kwenda Arusha wala kutoka Arusha kwenda Moshi.