Mwalimu mkuu jela miezi 12 kwa rushwa ya ngono

Muktasari:

Mahakama ya Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza, imemhukumu mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Jabal Hirah, Mwatanda Omari (37) kifungo cha miezi 12 jela kwa kosa la kuomba rushwa ya ngono.

Mwanza. Mahakama ya Wilaya ya Ilemela jijini Mwanza, imemhukumu mwalimu mkuu wa Shule ya Msingi Jabal Hirah Mwatanda Omari (37) kifungo cha miezi 12 jela kwa kosa la kuomba rushwa ya ngono.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatano Mei 15, 2019 na mkuu wa Takukuru mkoa wa Mwanza, Emmanuel Stenga imedai kuwa  hukumu hiyo imetolewa leo na Hakimu Mkazi wa manispaa ya halmashauri ya wilaya ya Ilemela, Abesizya Kalegeya baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa mahakamani hapo.

Awali upande wa Jamhuri ukiongozwa na mwanasheria wa Takukuru, Placidia Rugalema umedai kuwa mwalimu huyo alitenda kosa hilo Machi 9, 2017 kwa kumuomba ngono mzazi wa mwanafunzi aliyekuwa anaomba uhamisho wa mtoto wake kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam.

Mwalimu mkuu huyo ambaye ndiye mwenye mamlaka ya kujaza fomu ya uhamisho alitaka apewe ngono ndipo aweze kujaza fomu hiyo kinyume na kifungu cha 25 cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa namba 11/2007.

Mshtakiwa kwa upande wake aliiomba mahakama imsamehe kwa kuwa hakutenda kosa hilo kwa kukusudia, hata hivyo mahakama ilimpa adhabu ya kwenda jela miezi 12 au kulipa faini ya Sh2.5 milioni ambapo alikosa fedha hizo na kwenda jela.