Mwanamke aliyenusurika kifo kwenye mashambulizi mawili

Sunday January 20 2019

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Halikuwa jambo ambalo Tracy Wanjiru alitarajia lingetokea siku ya Jumanne alipokuwa akienda kazini kwenye jengo la Hoteli ya DusitD2, Nairobi nchini Kenya.

Wanjiru (28) meneja wa saluni kwenye jengo hilo akiwa kazini hana hili wala lile ghafla ukasikika mlio wa bomu na mwendelezo wa risasi, jambo lililomkumbusha miaka sita iliyopita aliponusurika kifo kwenye shambulio la Westgate Mall mnamo Septemba 2013.

Anasema kuwa hakuwaza sana hali iliyokuwa inatokea kwenye jengo la DusitD2 bali aliwaza hali ilivyokuwa Westgate alipokuwa na ujauzito wa miezi sita pale kikundi cha kigaidi cha Al-Shabaab kilipofanya mashambulizi. “Nimenusurika mara ya pili baada ya ile ya mwaka 2013, nilikuwa nikifanya kazi pale washambuliaji walipovamia , haikuwa rahisi kama leo. Yote naweza kusema ninamshukuru Mungu, “aliiambia Nairobi News katika mahojiano maalumu.

Anasema tofauti na Westgate ambako alikuwa mbali kidogo na wavamizi, Riveside nilikuwa karibu kabisa na washambuliaji ila alitumia uzoefu aliokuwa nao kujiokoa.

Mshituko wa kwanza

Wanjiru anasema dakika chache baada ya saa 3:00 asubuhi siku ya Jumanne, alisikia mlipuko wa bomu na mirindimo ya risasi karibu na mahali ambapo alifanya kazi.

Anasema alijaribu kusikiliza kwa makini kama anachokisia ni bomu... naam akajiridhisha ni bomu na akajaribu kuchungulia nje akaona tayari kuna taharuki.

“Mlipuko ulikuwa wa nguvu na ulichukua dakika kadhaa, nilirudi saluni na nikamwambia mwenzangu kuwa tumeshambuliwa , tulijaribu kukimbia lakini tulisikia sauti na kelele kila mahali huku risasi zikiendelea kufyatuliwa tukajificha, ” anasema.

Anasema alijiambia moyoni, hawezi kupona na kifo tena kama ilivyotokea huko nyuma. Kifo changu kipo karibu nami...Niliona mabaki ya miili ya binadamu katikati ya moto

Anasema kutokana na uzoefu alioupata kwenye mlipuko wa mwaka 2013 aliandika kwenye ukurasa wake wa facebook akiomba msaada.

“Nikiwa nimejificha niliandika kwenye ukurasa wa Facebook na mitandao mingine ya kijamii kuomba msaada na kuwaomba watu watoe taarifa Polisi kuwa tumevamiwa, ”anasema.

Shambulio la Westgate

Takribani watu 15 waliuawa na watu wenye silaha waliotambulika kutoka kikundi cha kigaidi cha Al Shabaab, ambao walivamia eneo la ofisi la 14 Riveside Jijini Nairobi.

Tukio hilo lililotokea, Januari 15, 2013 na lilianza saa 3:30 asubuhi, ambapo makundi ya wafanyakazi wapatao 150 waliokolewa na wengine wengi wakisalia ndani wakipewa huduma ya kwanza kutokana na majeraha.

Ofisa mmoja wa serikali ya Marekani aliuambia mtandao wa Reuters kuwa miongoni mwa watu hao waliouawa, mmoja ni raia wa Marekani.

Ikumbukwe kuwa nchi ya Kenya imekuwa ikivamiwa ikilengwa na kundi la Al Shabaab tangu mwaka 2013, ambapo ilivamia jengo la kibiashara la Westgate Jijini Nairobi na kuua watu 67.

Pia, shambulio lingine lililotekelezwa mwaka 2015 katika Chuo Kikuu cha Garissa, ambapo wanafunzi 150 waliuawa huku kikundi hicho kilijigamba kuwa ni kulipiza kisasi kwa kile walichodai nchi hiyo kuingilia mgogoro wa Somalia, baada ya kupeleka wanajeshi wake wa kulinda amani nchini humo.

Mbali ya Wanjiru aliyetumia mitandao ya kijamii kupitia simu yake kuomba msaada Lisa Bridgett anaamini kuwa alinusurika kifo kwenye shambulizi la magaidi lililotokea Manchester nchini Uingereza, Agosti, mwaka juzi. Mwanamke huyo alisema anaamini alinusurika kwa sababu alikuwa akizungumza kwenye simu aina ya iPhone wakati bomu lilipolipuliwa.

“Simu ilipunguza kasi ya mlipuko kunifikia kwani ilipasuliwa yenyewe na mimi kupata majeraha maeneo mbalimbali, ”aliandika Lisa kwenye mtandao wa Facebook.

Mama huyo mwenye miaka 45 alikuwa amekwenda kuhudhuria onyesho la mwanamuziki Ariana Grande wakati mshambuliaji wa kujitoa muhanga Salman Abedi alipojilipua.

“Bomu lilijeruhi na kukivunja kabisa kidole changu cha kati, lakini halikunifikia vizuri baada ya kushambulia zaidi simu, ”alisema. Mumewe Lisa, Steve Bridgett (45), alisema mkewe ana bahati alikuwa akizungumza na simu wakati shambulio linatokea licha ya kupata majeraha maeneo mbalimbali ya mwili, bado alinusurika kifo.

Alisema alipata majeraha makubwa miguuni, ikiwamo mguu kuvunjika, kidole na majeraha madogomadogo mwilini, ambapo kama shambulio lisingelenga simu angeumia zaidi.

Shambulio la Manchester

Takriban watu 19 walipoteza maisha na wengine 59 kujeruhiwa kufuatia shambulio la bomu la kujitoa mhanga lililowalenga vijana waliokuwa wakitoka kwenye tamasha la muziki kwenye uwanja wa Manchester nchini Uingereza.

Shambulio hilo lilitokea Mei 23, mwaka juzi saa 4:35 kwenye shoo ya mwanamuziki wa Marekani, Ariana Grande.

Baada ya mlipuko huo kusikika, vijana waliokuwa wakitoka kwenye uwanja huo unaochukua watu 21,000, walianza kukimbia hovyo ambapo mashuhuda walisema ilikuwa kama eneo la vita.

Advertisement