Mwandishi wa Mwananchi ashikiliwa Polisi

Muktasari:

  • Polisi mkoani Mwanza inamshikilia Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Jonathan Mussa kuhusiana na taarifa za watu kukamatwa na vichwa vya binadamu zilizosambaa eneo la Nyakato, Mwanza
  • MCL ni  wazalishaji wa magazeti ya Mwananchi, MwanaSpoti, The Citizen na MCL Digital 

Mwanza. Mwandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) mkoani Mwanza, Jonathan Musa anashikiliwa na polisi kwa mahojiano kuhusiana na taarifa za watu kukamatwa na vichwa vya binadamu zilizozagaa na kuzua taharuki miongoni mwa wakazi wa eneo la Nyakato jijini humo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Jumanne Muliro amesema Mwandishi huyo aliyekamatwa jana jioni Jumatano Februari 20, 2019 ni kati ya watu kadhaa wanaohojiwa baada ya kushikiliwa eneo la Nyakato walipokuwa wakifuatilia ukweli kuhusu taarifa hizo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai mkoa (RCO) wa Mwanza, Faustine Mafwere, Jonathan anashikiliwa kwa kosa la kumpiga picha alipokuwa akizungumza na wananchi waliokuwa nje ya kituo cha polisi Nyakato kufuatilia suala hilo akiwataka watawanyike.

Licha ya RCO awali kuahidi kumwachia huru Jonathan baada ya kuandikisha maelezo, baadaye alibadilika kwa kusema hakuna askari wa kutosha wa kuwachukua maelezo watu wote waliokamatwa kwenye tukio hilo ambao hata hivyo hakutaja idadi yao.

Endelea kufuatilia Mwananchi kujua kitakachojiri