Mwinyi, Kikwete wamfagilia Rais John Magufuli

Muktasari:

Rais wa awamu ya pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amesema kila Mtanzania aweke nia ya kumsaidia Rais John Magufuli siyo kwa ajili yake, bali kwa maslahi ya nchi na kila mmoja huku Rais Kikwete akimsihi aendelee kujenga umoja wa kitaifa.

Dar es salaam. Rais mstaafu wa awamu ya pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi amesema kila Mtanzania aweke nia ya kumsaidia Rais, John Magufuli siyo kwa ajili yake bali kwa maslahi ya nchi na ya kila mmoja.

Ameyasema hayo leo Jumapili  Mei 19, 2019 katika Mashindano ya 20 ya kusoma na kuhifadhi Quuran Afrika, yaliyofanyika katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na yameandaliwa na taasisi ya Al-Hikma.

Amesema licha ya kuwa mkutano huo ni wa Quran si wa siasa, lakini anawiwa kusema miaka mitano ipite apewe kura ili aendelee kuleta maendeleo kusudi miaka mitano ijayo imalizike kwa maendeleo.

“Nchi haina ndege, leo ina ndege, nchi ina reli ya kusuasua leo ina reli ya fahari ya kujivunia ndani ya miaka mitano. Ndani ya miaka mitano watu wameshikana wapo wengi ... ameshikilia mwenzetu tumsaidieni,” amesema Mwinyi.

Amesema; “Kilichobaki ni mimi kumshukuru Rais sana kwa namna anavyotuongoza katika awamu ya tano, kila nikikaa hustaajabu, huona maendeleo makubwa ya gharama kubwa yanatendeka katika muda mdogo sasa kama lipo la kusema niseme Mwenyezi Mungu amjaalie kasi iliyopo isirudi nyuma iendelee hivihivi.”

Naye Rais wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete amesema Waislamu na Wakristo wanaishi katika nchi moja bila kubaguana kwa sababu ndiyo mazoea yao.

Amesema katika makazi mengi jijini Dar es Salaam hasa nyumba za kupanga,  wanaishi watu wa dini tofauti huku akitolea mfano kuwa chumba cha kwanza huenda akawa Mkristo, cha pili Mwislamu na watatu ambaye hajafungamana na dini yoyote.

“Hivyo wewe Rais kuja katika mashindano haya ni faraja kwetu faraja kubwa lakini faraja kubwa ni maneno uliyoyasema ya kusisitiza mshikamano baina ya Watanzania wa dini zote na madhehebu mbalimbali.”

Kikwete  alimalizia Salamu zake kwa kusema; “Mimi sina zaidi ya kusema ila ahsante sana endelea na moyo huo wa kujenga mshikamano wa Taifa letu na watu wake, mahali salama.”