VIDEO: Nape afunguka, atetea urais wa Magufuli

Muktasari:

Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amezungumzia mambo matatu kuhusu tamko lililotolewa na makatibu wakuu wawili wa zamani wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana huku akisema wanaodhani Rais John Magufuli hawezi kugombea urais mwakani wanapoteza muda wao.


Dar es Salaam. Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye amezungumzia mambo matatu kuhusu tamko lililotolewa na makatibu wakuu wawili wa zamani wa chama hicho, Yusuf Makamba na Abdulrahman Kinana huku akisema wanaodhani Rais John Magufuli hawezi kugombea urais mwakani wanapoteza muda wao.

Hata hivyo, hakuwa tayari kuzungumzia sauti zinazodaiwa kuwa za kwake zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii kwa madai suala hilo lina ujinai na kwamba anaviachia vyombo vinavyohusika.

Nape, ambaye amewahi kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa CCM akizungumwa na Mwananchi jana alisema anayedhani kuna uwezekano wa kumfanya Rais John Magufuli asiwanie nafasi hiyo mwaka 2020 anajisumbua kwa kuwa utaratibu wa CCM Rais aliyepo madarakani, huwania tena nafasi hiyo awamu ya pili.

Nape ametoa kauli hiyo huku kukiwa na hali ya sintofahamu baada ya Kinana na Makamba kumuandikia barua katibu wa baraza la ushauri la viongozi wastaafu wa CCM, Pius Msekwa wakidai kudhalilishwa kwa mambo ya uzushi, uongo na mtu aliyejitambulisha kuwa mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.

Walisema jambo hilo linahatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani ya chama hicho na nchi.

Makamba na Kinana waliokuwa watendaji wakuu wa chama hicho tawala katika awamu ya nne, Jumapili iliyopita walitumia katiba ya CCM, toleo la 2017 ibara ya 122 kuwasilisha malalamiko yao ambayo yamezua mjadala ndani na nje ya chama hicho.

Tangu malalamiko hayo yalipotolewa, hakuna kiongozi yeyote wa CCM aliye madarakani amejitokeza kuyazungumzia na Mwananchi limekuwa likiwatafuta mara kadhaa bila mafanikio.

Mbali na tamko hilo, hivi karibuni katika mitandao ya kijamii zimesambaa sauti zikidaiwa kuwa za Nape, Kinana na baadhi ya makada wa chama hicho wakizungumzia tamko hilo kuliunga mkono.

Lakini akizungumza na Mwananchi jana, Nape alisema “sauti zinazoenea mitandaoni nimezisikia, uchezeaji wa sauti za watu ina sheria katika nchi yetu na ndani yake kuna jinai.”

“Kwa hiyo ushauri wangu tuviachie vyombo vinavyohusika na kusimamia sheria zinazolieleza jambo hili na vitatwambia ni nini kinachoendelea, ila wanaolijadili waweke akiba ya maneno ili wasiwe sehemu ya jinai.”

Alisema katika mjadala huo kumetokea suala la uchaguzi mkuu wa 2020 ndani ya CCM “watu wote wanaodhani kuna uwezekano wa kumpinga Magufuli ndani ya CCM ni ambao ama hawaijui CCM vizuri au wameamua kuwa wanafiki.

“CCM ina utamaduni, mtu akipitishwa ngwe ya kwanza, ya pili anapita tu aidha litokee tatizo kubwa ambalo mpaka sasa hivi halijatokea. Wengine wanajua hili lakini wameamua kuwa wanafiki kwa maana ya kwamba wakidhani hivi ni kujimilikisha Magufuli. Magufuli ni wa CCM wote si wa watu fulani, wanafanya hivyo kuonekana wanamtetea Magufuli ili awe mgombea,” alisema.

Akitolea mfano miaka ya nyuma, Nape alisema mwaka 2000, Rais mstaafu Jakaya Kikwete alisemwa atampinga Benjamin Mkapa (Rais wa Awamu ya Tatu) lakini hakuna kilichotokea.

“Mwaka 2010 Kikwete alitajwa angepingwa na Lowassa (Edward-waziri mkuu wa zamani) na sasa ametengenezwa mtu anaitwa (Benard) Membe, hilo haliwezekani labda apingwe nje ya CCM.”

“Nadhani watu wasiigawe nchi na wana CCM kwa kuleta ajenda ambayo siyo. Hapa kuna ajenda ya watu kulalamika kuwa wamechafuliwa. Huu utamaduni wa kuwasema watu waliostaafu utatutengenezea mazingira watu kuogopa kustaafu kwa kuogopa kusemwa. “

Aliongeza, “kama wana makosa ya kisheria wachukuliwe hatua na kisheria na kama makosa ya kibinadamu tutafute namna ya kuyashughulikia.”

Alipoulizwa sababu za sauti hizo kusambazwa, Nape alisema ni kutokana na kukaribia kwa uchaguzi, “kumekuwa na utaratibu linaibuka kundi na kusema watu wanataka rais asiendelee, umekuwa kama mchezo wa kawaida hivi.”