Ndalichako azindua kongamano kujadili upatikanaji wa nishati barani Afrika

Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia,Profesa Joyce Ndalichako(kushoto) akizungumza jambo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela(NM-AIST),Profesa Emmanuel Luoga wakati wa kongamano la kimataifa la nishati endelevu na miundombinu ya maji mkoani Arusha .Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

Kongamano la kujadili nishati endelevu barani Afrika limezinduliwa mkoani Arusha na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako

Arusha. Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia nchini Tanzania, Profesa Joyce Ndalichako amefungua kongamano la kimataifa kujadili mikakati ya kuwezesha upatikanaji wa nishati endelevu na miundombinu ya maji barani Afrika.

Akizungumza katika kongamano hilo la siku tano leo Jumatatu Agosti 12,2019 katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Nelson Mandela(NM-AIST), Waziri Ndalichako amesema maendeleo yeyote yanategemea uwepo wa nishati na uhakika wa maji.

Amesema Tanzania imejikita katika kujenga uchumi wa viwanda ambao unategemea zaidi shughuli za utafiti zinazofanywa na taasisi mbalimbali.

Awali, Makamu Mkuu wa Chuo NM -AIST, Prosefa Emmanuel Luoga amesema ushirikiano kati ya chuo hicho na taasisi ya utafiti ya iTEC kutoka Korea umefanikisha kongamano hilo la tatu nchini.