Ndege ya ATC iliyotekwa kushinikiza Nyerere ajiuzulu-10

Muktasari:

Katika toleo lililopita, tuliona jinsi Kapteni Deo Mazula, ambaye alikuwa rubani wa ndege ya Shirika la Tanzania (ATC) iliyotekwa wakati ikijiandaa kupaa kutoka Uwanja wa Ndege wa Mwanza, alivyotoa ushahidi ambao kwa kiasi kikubwa ulitumika kuwatia hatiani vijana watano waliohusika katika utekaji huo. Leo tunaendelea na jinsi waandishi na wachambuzi walivyozungumzia tukio hilo na kesi kwa ujumla.

Mbali na rubani Deo Mazula kutoa ushahidi katika kesi hiyo ya aina yake iliyofanyika Uingereza, mashahidi wengine wa upande wa mashtaka, ambao waliitwa kutoka Tanzania, ni wahudumu w ndege za ATC, H. Khan na Abdallah Idi, ambao pia walithibitisha ushahidi wa Kepteni Mazula na msaidizi wake, Oscar Mwamaja.

Khan, muhudumu wa kike katika ndege hiyo alielezea jinsi watekaji walivyowataka abiria kufumba macho yao na kuweka mikono yao vichwani na kutishia kwamba ikiwa yeyote angekaidi amri hiyo “angeadhibiwa vibaya sana”.

Aliiambia mahakama hiyo kuwa yeye mwenyewe, alitishwa kwa kisu.

Lakini, mjadala mkubwa uliibuka baada ya hukumu ya kesi hiyo.

Kitabu ‘Terrorism and International Law’ kilichohaririwa na Maurice Flory na Rosaly Higgins, katika ukurasa wake wa 340 kinasema: “Awali ilionekana kana kwamba hii ni kesi ya kawaida, ambayo hukumu yake ilitegemea sana sheria ya utekaji ya mwaka 1971 ya Uingereza (The Hijacking Act, 1971), lakini kutokana na utetezi uliotolewa na baadhi ya washtakiwa uliifanya kesi hiyo isiwe ya kawaida.”

Kitabu hicho kinasimulia kwamba watekaji hao walilazimika kufanya tukio hilo ili “kujiondoa wao na familia zao kutoka ardhi ya Tanzania, kwa sababu walihisi kuwa walikuwa wanakandamizwa na Serikali.

“Tatizo kwao lilikuwa ni namna ambayo wangeondoka Tanzania. Njia dhahiri ambayo wangeweza kuitumia ni anga, lakini kwa kutumia njia hiyo wangelazimika kupitia taratibu zote za kawaida za uhamiaji ikiwa tu walitaka kuondoka (Tanzania) kwa njia ya anga.

Mwandishi wa kitabu hicho anasema wazo likawajia la kutengeneza mipango ya kuondoka kwa kwa kuiteka ndege inayotoa huduma ndani ya nchi.

“Utekaji [nao] ungekuwa ni jambo gumu sana kulifanikisha iwapo watekaji hawangemshirikisha angalau mmoja wa wafanyakazi wa ndege hiyo ambaye angekuwa tayari kushiriki,” anaandika mwandishi huyo.

Dhana ya kuwa na mshiriki angalau mmoja ilijitokeza pale Musa Memba alipotoa utetezi wake. Katika ushahidi wake, Musa Memba alidai kwamba rubani Mazula alikuwa mshirika wake wa siri na kwamba alikuwa na habari za mpango mzima wa kuiteka ndege yake.

Kitabu Terrorism and International Law kinaeleza kuwa Musa Memba alieleza katika ushahidi wake kuwa alishiriki kula njama na rubani wa ndege hiyo na kwamba Mazula alikuwa tayari kusaidia kwa sababu naye alishaona mustakabali wa maisha yake ya kikazi nchini Tanzania haukuwa.

Anasema katika kitabu hicho kuwa Mazula alikuwa akiwaza sana kwenda kufanya kazi kwenye mashirika ya ndege ya Mashariki ya Kati kuliko kuendelea kufanya kazi ATC.

Hata hivyo, Kepteni Mazula alikanusha madai hayo akisema kuwa hajui lolote kuhusu mpango wa watekaji hao. Alisema katika maisha yake yote hakuwahi kumsikia wala kukutana na Musa Memba kabla ya utekaji huo kufanyika na aliamini kwamba watekaji walinuia kuilipua ndege kama matakwa yao yasingesikilizwa.

David Howell, mwenyekiti wa Kamati ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Mataifa (nchini Uingereza), akikaririwa na gazeti ‘Independent la Uingereza la Jumatano ya Agosti 28, 1996 alisema vijana hao walifanya utekaji kwa kuwa ndio ilikuwa njia rahisi ya kupata hifadhi ya ukimbizi, kitu ambacho alisema ni hatari.

“Kuteka ndege ni uhalifu mbaya na wakati mwingine ni mauaji,” anasema Howell katika mahojiano hayo.

“Kama watu watasikia fununu kwamba njia rahisi ya kupata hifadhi ya kisiasa ni kuteka ndege, halafu unashtakiwa na kufungwa jela miaka mitatu halafu uachiwe, na hapo ujikute uko katika nchi uliyotaka, hiyo itakuwa hatari sana kwa sera yote ya hifadhi ya kisiasa.”

Itaendelea kesho