Ndugai azungumzia mahakama inayotembea

Muktasari:

Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wakati wazo la kuanzishwa kwa mahakama inayotembea linapelekwa bungeni alipata changamoto nyingi ikiwemo kugoma kupitisha sheria ambayo hawaifahamu


Dar es Salaam. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema wakati wazo la kuanzishwa kwa mahakama inayotembea linapelekwa bungeni alipata changamoto nyingi ikiwemo kugoma kupitisha sheria ambayo hawaifahamu.

Ameyasema hayo leo Februari 6, 2019 katika maadhimisho ya siku ya sheria nchini yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Julius Nyerere jijini hapa.

“Waliomba hadi kupelekwa ziara ili wakaone jinsi mahakama hiyo ilivyo kwa sababu ni kitu kigeni, hata mimi nilikuwa sielewi lakini hatimaye hata mimi nimeona kwa macho kumbe ni kweli nawapongeza sana mahakama kwa jambo hili, hongereni sana,” amesema Ndugai.

“Kama Bunge tutaendelea kuhakikisha hatukatishi katika mstari wa mahakama na tukikosea tunaomba mtukumbushe haraka sana ili turudi katika mstari tunaotakiwa kuwa ili kuhakikisha kuwa uhuru wa mahakama unalindwa pale bungeni na hata nje.”

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema ongezeko la majaji wa Mahakama Kuu na Rufani  linatakiwa kwenda sambamba na ongezeko la fedha hususani katika ununuzi wa magari, nyumba, samani, kompyuta mpakato  na fedha za uhamisho kutoka vituoni.

“Kutokana na hayo yote nyongeza ya fedha Sh11.95 bilioni zinahitajika kabla ya Juni Mwaka huu,” amesema.