Nicki Minaj afuta maonyesho yake Saudi Arabia kutetea wanawake

Muktasari:

Nyota huyo wa muziki wa rap alikuwa atumbuize katika tamasha la utamaduni la Jeddah pamoja na wasanii wengine maarufu wa Uingereza na Marekani


Nicki Minaj amefuta maonyesho yake nchini Saudi Arabia kutokana na kupinga ukiukwaji wa haki za wanawake katika nchi hiyo ya kifalme yenye msimamo wa kihafidhina, rapa huyo wa Marekani alisema jana Jumanne.

Ratiba ya Minaj kufanya onyesho katika jiji lililo magharibi la Jeddah wiki ijayo, ikiwa ni sehemu ya tamasha la utamaduni, iliamsha mijadala katika mitandao ya kijamii kuhusu ukiukwaji wa haki za binadamu kwenye nchi hiyo.

"Baada ya kutafakari kwa makini, nimeamua sitaendelea na onyesho langu katika (tamasha la utamaduni wa dunia la Jeddah) Jeddah World Fest," Minaj alisema katika taarifa yake iliyotumwa AFP na ofisa habari wake.

"Wakati sitaki kingine zaidi ya kuwapa burudani mashabiki wangu nchini Saudi Arabia, baada ya kujielimisha kuhusu masuala haya, naamini ni muhimu kwangu kuonyesha bayana kuwa naunga mkono haki za wanawake na uhuru wa kujieleza."

Minaj, anayejulikana kwa nyimbo zenye mashairi ya matusi na video za masuala ya ngono, alikuwa akitarajiwa kuwa kinara katika tamasha hilo wakati dola hiyo ya kifalme ikilegeza sheria za muda mrefu zilizokuwa zinabana burudani.

Wengine waliokuwa wmepangwa kutumbuiza ni mwanamuziki wa Uingereza, Liam Payne na Mmarekani DJ Steve Aoki.

Taasisi ya haki za binadamu ya HRF ya New York iliandika barua ya wazi Ijumaa kwa Minaj ikimshauri ajiondoe katika tamasha hilo, ikimtaka akatae fedha za serikali na badala yake kutumia umaarufu wake duniani kushinikiza kuachiwa huru kwa wanawake waliofungwa nchini Saudi Arabia.

Shirika la Amnesty International limeelezea rekodi ya haki za bindamu nchini Saudi Arabia kuwa ni "mbaya sana", ikiongeza kuwa taifa hilo linaendelea na mkakati wa kuwamaliza wanaoikosoa serikali.

"Itaniuma hata kama mmoja wa mashabiki wangu akikamatwa au kupigwa kwa sababu ya kueleza hisia zake," Minaj alisema katika twiti yake Jumanne.