Ofisi ya Waziri Mkuu yawasilisha mapendekezo ya kufutwa kwa tozo

Wednesday May 15 2019

Ofisi , Waziri ,Mkuu ,yawasilisha, mapendekezo , kufutwa, tozo,Angela ,Kairuki

Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki akijibu hoja za wabunge waliochangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Ericky Boniphace 

By Sharon Sauwa, Mwananchi [email protected]

Dodoma. Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Angela Kairuki amesema wamewasilisha Wizara ya Fedha na Mipango mapendekezo ya tozo zinazotakiwa kuondolewa ili kuwezesha biashara kukua nchini.

Kairuki ameyasema hayo leo Jumatano Mei 15, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2019/2020.

Amesema ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Viwanda na Biashara na nyingine, wamekaa na kujadili kwa kina ili kuangalia changamoto ambazo ni vikwazo katika uwekezaji ili kuhakikisha kuwa kunakuwa na uwekezaji mkubwa na biashara kukua.

“Tayari ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Viwanda na Biashara imechukua hatua ya kupitia mapendekezo yote katika Road Map na Blue print ,”amesema.

Amesema Waziri Mkuu alishaitisha kikao Aprili 17 mwaka huu  lakini Jumamosi Mei 18 mwaka huu watakuwa na kikao kingine na Waziri Mkuu na wizara mbalimbali ili kupitia changamoto na vikwazo vyote ambavyo vimekuwa vikichangia biashara kutokua.

“Amesema tayari kuna tozo ambazo zimependekezwa kuondolewa. Tumeziwasilisha Wizara ya Fedha kupitia Task Force ya Wizara ya Fedha ya kuangalia maboresho ya kodi,”amesema.

Kairuki amesema wanaamini  kupitia Muswada wa Fedha utakaoletwa Juni wabunge wataweza kujionea mabadiliko.

“Waziri wa Afya kuptia TFDA (Mamlaka ya Dawa na Chakula) amependekeza kuzifuta tozo na kupunguzwa. Lakini pia zipo tozo katika bodi yetu ya maziwa, nyama na taasisi nyingine za kiserikali ikiwemo TBS,”amesema.

Kuhusu mabadiliko ya Sheria ya Uwekezaji, Kairuki amesema kuwa suala hilo wameliona na kwamba sheria hiyo ni ya muda mrefu wa zaidi ya miaka 22.

“Ukiangalia kuna mambo yaliyoasisiwa na kuakisiwa inawezekana hayaendani na mazingira ya sasa. Lakini pia kuangalia suala la ushindani na nchi nyingine,”amesema.

Amesema sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi  imepewa kipaumbele katika kuvutia wawekezaji.

Amesema wanafanya hivyo kwa kutambua kuwa asilimia 65.5 wameajiriwa katika kilimo.

Amesema pia wanatambua kuwekeza katika sekta za kilimo, mifugo na uvuvi kutaongeza tija na athari yake kwa wananchi ni kubwa.

 

Advertisement