Ofisi za wabunge wa CUF zaanza kupeperusha bendera ya ACT-Wazalendo

Muktasari:

 

  • Wakati wanachama wa CUF wakiendelea kumfuata Maalim Seif Sharif Hamad aliyehamia ACT-Wazalendo, ofisi za wabunge wa CUF zilizopo Magomeni jijini Dar es Salaam zimebadilishwa na kuwa ofisi za chama hicho, baadhi wagoma kufuata upepo

Dar es Salaam. Ofisi ya wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF) wanaomuunga mkono aliyekuwa katibu mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad zimebadilishwa na na kuwa ofisi za chama cha ACT- Wazalendo.

Leo Mwananchi Digital imetembelea ofisi hizo zilizopo Magomeni jijini Dar es Salaam na kukuta bendera ya ACT-Wazalendo ikipepea mbele ya jengo hilo, huku maandishi yaliyokuwa yameandikwa ubavuni mwa ukuta yaliyosomeka: “Ofisi za wabunge wa CUF’ yakiwa yamefutwa.

Akizungumzia mabadiliko hayo, mwanachama mpya wa ACT-Wazalendo ambaye alikutwa kwenye ofisi hizo, Mbarara Maharagande amesema jengo hilo sasa ni ofisi ndogo za ACT -Wazalendo na zitafanya shughuli za chama hicho.

“Ofisi hizi zilipangishwa na wabunge wanane wa CUF ambao walitimuliwa, sasa wao pia wamehamia ACT-Wazalendo na wametoa kibali kwambazitumike kwa chama hiki,” amesema Maharagande ambaye alikuwa naibu mkurugenzi wa habari wa CUF.

Amesema ofisi nyingi za matawi ya CUF ni nyumba za watu binafsi ambao walikuwa wanachama na baadhi yao wameamua kuhamia ACT-Wazalendo na kuzifanya nyumba zao kuwa ofisi za ACT-Wazalendo.

“Hii ni operesheni inayofanyika Dar es Salaam nzima, matawi yote ya CUF yatakuwa ya ACT-Wazalendo kwa sababu wananchi wameamua kumfuata Maalim Seif katika chama cha ACT- Wazalendo,” amesema Maharagande.

Mwananchi imetembelea mitaa mbalimbali ya Ilala, Kinondoni na Temeke na kubaini bado ofisi za CUF zinaendelea kutumiwa na chama hicho na baadhi ya wafuasi wa wameapa kutohama bali kuendelea na chama chao.

“Sisi tunaendelea na CUF yetu ndiyo maana unaona ofisi zetu bado zipo. CUF tuko imara, tutaendelea na shughuli zetu za kukijenga chama hasa wakati huu ambapo migogoro imekwisha,” amesema Omary Mkwisi, mjumbe wa mtaa wa Sokoine.