Ole Sabaya: Upinzani unaoisumbua CCM ni wa majungu adai haina mpinzani

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro Patrick Boisafi,akimshukuru Mkuu wa Wilaya ya Hai Lengai Ole Sabaya,kwa kutoa Gari kwa ajili ya Shughuli za Chama Wilaya ya Hai.

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya amesema upinzani nje ya CCM umeisha na umebaki wa majungu na fitina unaofanywa na baadhi ya wanachama wa chama hicho ndani ya chama.

 

Hai. Mkuu wa Wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya amesema upinzani unaokisumbua Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa sasa ni ule wa majungu na fitina unaofanywa na baadhi ya wanachama wa chama hicho.

Sabaya ambaye ni mjumbe wa kamati ya siasa ya CCM  wilayani humo, ameyasema hayo leo Mei 15 wakati akikabidhi gari aina ya Toyota Hilux Double  Cabin kwa Chama hicho ili kusaidia shughuli za chama.

Akikabidhi gari hilo kwa mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Patrick  Boisafi katika ofisi za CCM wilaya ya Hai, Sabaya amesema vyama vya upinzani vimeshakufa vifo vya kawaida kwa sababu yupo mtu ambaye amefanya mambo ya miujiza kwa kipindi cha miaka mitatu alichokaa madarakani (Rais John Magufuli).

"Upinzani nje ya CCM umeisha, tatizo lililobaki ni baadhi ya wanachama wa CCM ambao baada ya kuona upinzani umeisha wakaona kazi iliyobaki ni  kuhamishia upinzani wa majungu na fitina ndani ya chama. Hamna adui huko nje, mmeleta adui ndani na nimeyaleta hapa hadharani kwa sababu hayo majungu na fitina hawayafanyi kwenye vikao, wanayafanya hadharani.”

 “Waache majungu na fitina, msiende mkawaiga wale watu wa mataifa ambao mnawajua wameshindwa kufanya lolote kazi yao wana ubaya usiku na mchana.Tekelezeni majukumu ambayo kwayo mliiombea Serikali dhamana na mkifanya hivyo kamwe hayupo mtu wa kukitoa Chama Cha Mapinduzi madarakani,” amesema.

Kuhusu gari alilotoa, Sabaya amesema ni kwa ajili ya kusaidia kwenda maeneo mbalimbali kusimamia utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM na kutatua kero, tabu na shida za wananchi wa Hai.

“Mimi na baadhi ya wadau werevu na wenzangu serikalini tukajichangisha, tukaamua kwa ridhaa yetu kununua gari iliyokuwa mnadani kwa Sh 15 milion, tukaitengeneza na leo tunaikabidhi CCM."

“Tumeileta gari hii kama heshima kwa chama kutokana na kazi nzuri inayofanya. Hatupangiwi na mimi  sipangiwi, zamu hii nimeamua kuwapa Chama Cha Mapinduzi," amesema.

Sabaya ameahidi pia kutengeneza gari aina ya Land Cruiser ambalo linatumiwa na chama hicho wilaya ya Ha.

Naye mwenyekiti wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Boisafi amemshukuru Sabaya kwa uzalendo aliouonyesha wa kununua gari hilo na kulikabidhi kwa chama.

“Ameonyesha uzalendo wa kutosha, lakini zaidi ameonyesha kwamba yeye kweli ni kada wa Chama Cha Mapinduzi, namshukuru yeye binafsi na wale wengine alioungana naye kununua gari hili kwani wangeweza kununua likawa la kwao lakini wameamua kulitoa zawadi kwa CCM,” amesema.

Aidha, Boisafi ametumia nafasi hiyo kuwataka wanachama wengine wa CCM kuiga mfano alioufanya Sabaya na kuhakikisha hawaishii kwenye magari bali hata muda wao na hata kukipigania chama.

“Ukweli ni kwamba vya upinzani ni kama vile vimekata roho na upinzani umebaki ndani ya chama na sisi hatuko tayari kuona upinzani unakuwa ndani ya chama.Tutahakikisha upinzani huu unaotaka kujitokeza ndani ya chama tunaukata kungali asubuhi kwani katika uchaguzi wa Serikali za mitaa tunahitaji ushindi wa kishindo,” amesema.

Kwa upande wake, Katibu wa CCM Mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya amesema gari hilo limekabidhiwa kwa chama na kuitaka CCM wilaya ya Hai kulitumia kwa shughuli za chama na kuyafikia malengo yaliyokusudiwa.