Operesheni kusaka wauaji wa watoto Njombe yaanza

Njombe. Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Christopher Ole Sendeka amewahakikishia wananchi wa mkoani humo kwamba Serikali na vyombo vyake vya dola vimejipanga kukabiliana na aina yoyote ya matukio ya mauaji ya watoto.

Wakati Ole Sendeka akieleza hayo, Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Jeshi la Polisi, Nsato Marijani ambaye anaongoza kikosi kazi maalumu kilichotua kufuatilia matukio hayo, amesema hakuna mtu aliyeshiriki kutekeleza mauaji hayo atakayebaki salama.

“Iwe kwa hiari au kwa shari hili litakwisha tu, tupeni taarifa sahihi na za kweli, tumekuja kushirikiana nanyi,” alisema Marijani.

Ole Sendeka alitoa kauli hiyo jana mchana akiwa na Marijani wakati walipokuwa wakizungumza na wananchi wa Mji wa Makambako kueleza dhamira ya Serikali katika kukabiliana na matukio hayo ambayo yameshika kasi.

Mkuu huyo wa mkoa alisema mauaji hayo kwa asilimia kubwa yanahusiana na imani za kishirikina. Alisema baadhi ya watu wanaotafuta utajiri wanaamini kwamba wataupata kupitia viungo vya binadamu jambo ambalo alisema ni potofu na kuapa kwamba Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha linamalizika na wahusika wanachukuliwa hatua za kisheria.

Alitaja makundi ambayo yanatekeleza mauaji hayo kuwa ni ya waganga wa jadi wanaofanya ramli chonganishi, watu wanaokwenda kwa waganga wakiwa na lengo la kutafuta utajiri na kupigiwa ramli kuaminishwa imani potofu.

Vilevile, alisema kuna kundi la tatu ambalo ni la mtandao unaotumiwa na watu wa kundi la pili kwa ajili kutekeleza mauaji hayo.

“Tunafanya msako wa makundi hayo matatu, lakini kuna kafara zinatolewa na ndugu wenyewe katika kutafuta utajiri. Matajiri wanaotokana utoaji kafara za binadamu wenzao au mwanasiasa anayetekeleza mauaji haya ili kujinufaisha kwa masilahi binafsi, nasema hivi, tukikubaini tutakushughulikia bila woga wowote,” alisema Ole Sendeka.

Awatega viongozi wa Serikali

Mkuu huyo wa mkoa alisema katu hatakubali kuona mwendelezo wa matukio ya mauaji mkoani humo na alitoa agizo kwa viongozi kuanzia Serikali za mitaa, vijiji kata na wilaya kuhakikisha hawamfumbii macho mtu yeyote atakayebainika kuwa na viashiria vya vitendo hivyo.

“Haya matukio Njombe tuseme imetosha. Ninaagiza viongozi kuanzia mtaa, kijiji na kata fanyeni msako na katika hili, nataka hata aliyefariki mwaka jana au mwaka juzi kwa mtindo kama huu lazima wahusika wote wasakwe popote walipo na siyo kwa tukio hili tu,” alisema Ole Sendeka.

Alisema hakuna kiongozi atakayebaki salama wakati eneo lake kuna mtu amekatishwa uhai wake kwa imani za kishirikina au kuuawa kwa namna yoyote ile.

Marijani aweka msisitizo

Akitoa ufafanuzi, Kamishna Marijani aliwataka wananchi kutoa ushirikiano wa dhati katika suala hilo bila hofu yoyote huku akibainisha kwamba vitendo hivyo lazima vikome.

“Hakuna atakayebaki salama kwa wale waliohusika na mauaji haya. Tumekomesha matukio makubwa yaliyowahi kutokea hapa nchini kama vile mauaji ya albino,” alisema Marijani.

Mkazi wa Makambako, Rahma Mwangile alisema matukio hayo yanahusishwa zaidi na wafanyabiashara wanaotafuta utajiri kwa njia za haramu.

“Mwenendo wa matukio haya yanafanywa na wafanyabiashara kwani huku kwetu wengi wanaendesha biashara zao kwa kutoa kafara, kwa kutoa uhai wa binadamu na hayajaanza leo,” alisema.