VIDEO: Pacha wa Kagera walioungana kurejea Tanzania Mei

Friday March 15 2019

By Nasra Abdallah, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Pacha waliokuwa wameungana, Marines na Anisia Benatus wanatarajiwa kurejea nchini kuanzia miezi miwili ijayo baada ya operesheni yao kufanikiwa huko nchini Saud Arabia.

Watoto hao waliozaliwa Januari 29, 2018 wilayani Missenyi mkoani Kagera, walisafirishwa kwenda nchini humo Agosti mwaka jana baada ya balozi wa Saud Arabia kuwatembelea katika Hospitali ya Muhimbili walipokuwa wamelazwa.

Hayo yamesemwa jana Machi 14, 2019 na balozi huyo wa Saudi Arabia nchini, Mohamed Mansour Almalik, wakati wa hafla ya chakula cha pamoja na madaktari tisa waliokuja kutoa msaada wa matibabu ya upasuaji kwa watoto ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia maendeleo ya watoto hao. 

Balozi Almalik amesema watoto hao kadri siku zinavyozidi kwenda afya zao zinaimarika na kilichobaki ni kuwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa muda huo wa miezi miwili kabla hawajarejea nchini.

Alifafanua kwamba lengo la kukaa chini ya uangalizi ni kuhakikisha wanaporejea nchini hawapatwi na tatizo lolote na kuwaomba Watanzania kuwa na subira kwa kuwa wapo katika mikono salama.

Akielezea kuhusu operesheni yao amesema ilikuwa na ugumu kidogo na ilichukua takribani saa 14 hadi kuisha kutokana na namna walivyokuwa wameungana.

Naye balozi wa Tanzania nchini Saud Arabia, Balozi Hemed Mgaza, amesema alifanikiwa kuwatembelea watoto hao na anashukuru kuwakuta wameanza kutoa sauti na wanacheza kama watoto wengine walio katika umri wao.

Katika hatua nyingine akizungumzia ujio wa madaktari hao, balozi Al Malik amesema ulikuwa ni wa mafanikio ambapo kwa muda wa wiki moja waliyokaa nchini wamefanyia watoto 25 operesheni mbalimbali ikiwemo ile ya njia ya mkojo.

Naye kiongozi wa msafara wa madaktari hao, Profesa Zakaria Habib, amesema mbali ya kutoa huduma za afya pia wametoa semina kwa madaktari wa watoto na kushukuru ukarimu walioonyeshwa kwa kipindi chote. Mwisho.

Advertisement