Padri atoa neno kwa Serikali juu ya matukio ya kikatili Rombo

Muktasari:

  • Paroko wa Parokia ya Usseri, Padri Emmanuel Liyimo ameitumia siku ya leo ya Jumapili kukemea matukio yanayoendelea wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro na kuiomba Serikali kuchukua hatua zaidi kukomesha vitendo hivyo

Rombo. Viongozi wa dini wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro wamelaani mauaji ya kikatili yanayoendelea wilayani humo, ikiwemo watu kuchinjwa na wengine kupigwa hadi kufa.

Akitoa mahubiri leo Jumapili Februari 17, 2019, katika Parokia ya Usseri, paroko wa kanisa hilo, Padri Emmanuel Liyimo amesema ipo haja ya Serikali kutumia nguvu za ziada kupambana na matukio yanayotokea wilayani humo ambako watu wanauliwa bila hatia.

katika misa ya ibada ya kwanza, ambayo imeongozwa na padri huyo, amesema tukio lililotokea juzi Februari 11, 2019 katika Kijiji cha Lessoroma la kuuawa mwanamke mmoja aitwaye Adelaide Onesmo ni tukio la kinyama na halipaswi kufumbiwa macho katika jamii.

Amesema wananchi katika wilaya hiyo wameendelea kuchukua sheria mkononi kwa kutekeleza mauaji huku ubakaji na ulawiti ukiendelea kushamiri wilayani humo.

"Haya mauaji yanayofanywa katika tarafa hii ya Usseri pamoja na sehemu nyingine hakika hizi damu za watu zinazomwagika zitawalilia watu wa Usseri," amesema paroko huyo.

Adelaide aliuliwa Februari 11, 2019 na wanawake wenzake wanaodaiwa walikua sita, kwa madai kuwa mwanaye wa kiume anayesoma darasa la sita Shule ya Msingi Kiraro aliiba chakula nyumba ya jirani na kukila baada ya kupata njaa kwa muda mrefu.

Mwili wa mwanamke huyo, umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Karume wilayani humo.