Polisi Tanzania wamwachia Halima Mdee

Muktasari:

  • Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama kikuu cha upinzani nchini humo (Bawacha), Halima Mdee aliyekuwa akishikiliwa na Polisi mkoani Kagera nchini Tanzania limemwachia kwa dhamana.

Bukoba. Polisi mkoani Kagera nchini Tanzania limemwachia kwa dhamana Mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee.

Mdee ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa chama kikuu cha upinzani nchini humo (Bawacha) alikamatwa jana jioni Jumapili Julai 14, 2019 na polisi mkoani humo mara baada ya kumalizika kwa kikao cha ndani cha wanawake mkoani Kagera.

Mwenyekiti wa Bawacha mkoani Kagera ambaye pia ni Mbunge wa Viti Maalumu Conchesta Rwamulaza akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Julai 15, 2019 amesema Mdee ameachiwa kwa dhamana.

Taarifa iliyotolewa na Chadema kupitia akaunti yake ya Twitter  imesema, “Hatimaye Jeshi la @tanpol mkoani Kagera wamemwachia @halimamdee kwa dhamana, akidhaminiwa  na watu wawili na kutakiwa kuripoti kituoni hapo baada ya mwezi mmoja au wakati wowote polisi watakapomhitaji. Tunawashukuru wote waliopaza sauti kupinga na kulaani vikali kitendo hicho.”

Leo mchana, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Tanzania kilitoa wito kwa jeshi la polisi kumwachia huru mbunge huyo au kumfikisha mahakamani mara moja.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga alisema tukio la kuzuiliwa kwa mikutano ya wapinzani ni mwendelezo wa ukandamizaji wa haki za kisiasa hapa nchini kwa mwaka wa tatu sasa.

"Tunalitaka jeshi la polisi kumpatia dhamana Mdee na kumfikisha mahakamani badala ya kumshikilia bila kufuata taratibu za kisheria za kuwafikisha mahakamani watuhumiwa," alisema Henga.