Profesa J asimulia bungeni jinsi alivyopambana akatangazwa mbunge

Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule akichangia bungeni mjadala wa kupitisha makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais (Tamisemi) na Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) kwa mwaka wa fedha 2019/2020, jijini Dodoma leo. Picha na Edwin Mjwahuzi

Muktasari:

  • Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule maarufu ‘Profesa J’ amesema nguvu ya wananchi ilisababisha tume kumtangaza kuwa mbunge kwani magari ya CCM yalikuwa yanaingia na kutoka bila kutangaza matokeo.

Dodoma. Mbunge wa Mikumi (Chadema), Joseph Haule maarufu ‘Profesa J’ leo ameeleza yaliyotokea wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na kutangazwa kuwa mbunge.

Amesema kama si nguvu ya wananchi wa Mikumi huenda asingetangazwa kuwa mbunge licha ya kuwa alishinda uchaguzi huo.

Akichangia katika hotuba mbili za ofisi ya Rais Tamisemi na utumishi na utawala bora bungeni jioni ya leo, mbunge huyo ameitaja tume ya taifa ya uchaguzi kuwa ndiyo kikwazo cha yote.

Mbunge huyo ambaye pia ni msanii wa muziki wa Hip hop amedai tume hiyo imekuwa ikifanya vitu kinyume ikiwamo kuwatangaza wagombea wa CCM kuwa wameshinda hata kama kura zao ni chache kuliko upinzani.

"Tume ya taifa itende haki, anayestahili kutangazwa tunaomba atangazwe siyo kama mnavyofanya, vinginevyo hatutakubali na mjifunze kwa nchi za wenzetu kinachowatokea baada ya wananchi kuamua," amesema Haule.

Ametolea mfano kuwa leo Mahakama ya Mbeya imemtangaza diwani wa Chadema kuwa mshindi wakati tume ilikuwa imemtangaza  diwani wa CCM.

Amesema kama tume hiyo itatenda haki, hakutakuwa na malalamiko kwa pande zote kwani demokrasi itakuwa imesimama mahali pake.

Katika hatua nyingine, mbunge huyo ameomba tume ya kwenda kuchunguza wananchi 10 ambao wamepotea na hawajulikani walipo hadi sasa.

Amesema watu hao wanasadikiwa kupotea katika hifadhi ya Mikumi lakini hakuna chochote kinachosemwa kuhusu watu hao hivyo jambo hilo linatia shaka.