Profesa Kabudi atoa ufafanuzi kauli yake kuhusu Azory Gwanda

Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema alinukuliwa vibaya kuhusu mwandishi wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda.

Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje nchini Tanzania, Profesa Palamagamba Kabudi amesema alinukuliwa vibaya kuhusu mwandishi wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda.

Profesa Kabudi ametoa ufafanuzi huo leo Alhamisi Julai 11, 2019, akidai alinukuliwa nje ya muktadha wakati akihojiwa jana katika kipindi cha Focus on Africa kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), alipoulizwa swali kuhusu kutoweka kwa Azory tangu Novemba, 2017.

Katika tamko lake kwa vyombo vya habari alilolitoa leo, Profesa Kabudi amesema, “Mpaka sasa hakuna uthibitisho kuwa Azory yuko hai au amefariki. Vyombo vya ulinzi na usalama vinaendelea kuchunguza tukio hilo na matukio mengine yaliyotokea katika machafuko ya Kibiti, Pwani yaliyosababisha ama watu kadhaa kupoteza maisha au kupotea.”

Azory alitoweka katika mazingira ya kutatanisha kwa kuchukuliwa na watu wasiojulikana  ambapo mpaka sasa hajapatikana.

Waziri huyo ametoa ufafanuzi kutokana na maelezo aliyoyatoa katika kipindi cha BBC Focus on Africa ambako amekaririwa akisema Azory ni miongoni mwa wananchi waliopotea na kufariki.

Alikuwa akijibu swali la mwandishi, Peter Okwoche, aliyemuuliza kuhusu kupotea kwa Azory na mahali alipo.

“Hilo lilikuwa ni miongoni mwa mambo yaliyoumiza ambayo Tanzania ilipitia. Katika eneo la Rufiji, siyo Azory Gwanda peke yake aliyepotea na kufariki. Zaidi ya polisi 10 walipigwa risasi na kufariki kikatili, viongozi wengi wa vijiji  wa CCM ambacho ni chama tawala, waliuawa Rufuji.”

“Tunamshukuru Mungu tuliweza kudhibiti aina hiyo ya siasa kali ambazo sasa zimehamia Kaskazini ya Msumbiji na wiki iliyopita Watanzania 10 waliuawa. Kwa hiyo Azory ni miongoni mwa Watanzania wengi waliouawa na kupotea katika eneo hilo,” amesema Profesa Kabudi katika mahojiano hayo.

Kwa ujumla taarifa za kutoweka kwa Azory zilitangazwa kwa mara ya kwanza Desemba 7, 2017 katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa habari. Mkutano huo ulifanyika ofisi za makao makuu ya MCL zilizopo Tabata Relini, Dar es Salaam.

Baadaye, MCL iliendesha kampeni ya kumtangaza Azory kwenye kurasa za mbele za magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na mitandao yake kwa kipindi cha siku 100. Licha ya juhudi zote hizo, hadi Machi 1, 2018 wakati zilipotimia siku 100 hakuna taarifa iliyotolewa na chombo chochote kuhusu mahali Azory alipo, hadi leo hakuna taarifa zozote.