Profesa Ngowi azungumzia uchumi wa viwanda, maendeleo ya watu

Profesa wa  Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi

Muktasari:

  • Profesa wa  Chuo Kikuu cha Mzumbe, Honest Ngowi amesema kuna haja ya kuunganisha uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu ili matokeo ya uchumi huo yawaguse wananchi moja kwa moja

Dar es Salaam. Profesa wa  Chuo Kikuu cha Mzumbe nchini Tanzania, Honest Ngowi amesema kuna haja ya kuunganisha uchumi wa viwanda na maendeleo ya watu ili matokeo ya uchumi huo yawaguse wananchi moja kwa moja.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Julai 4, 2019  jijini Dar es Salaam wakati akichambua bajeti ya serikali kwa wakurugenzi wa asasi za kiraia kutoka mikoa mbalimbali nchini Tanzania

Amebainisha kuwa kwa bahati mbaya eneo la maendeleo ya watu halijafanyiwa kazi ya kutosha badala yake msisitizo mkubwa umewekwa kwenye maendeleo ya vitu kama ujenzi wa miundombinu.

“Tunaweza kujenga viwanda vingi lakini kama havigusi maisha ya watu haina maana. Maendeleo ni ya watu, kwa hiyo ni muhimu kuwekeza kwenye vitu kama elimu bora, afya na maji," amesema Profesa Ngowi.

Profesa Ngowi amesema kuna haja ya kuwekeza kwenye ubunifu kwa sababu ndiyo mahitaji ya soko kwa sasa.

Msomi huyo amebainisha kuwa watu wanatakiwa kufundishwa ujuzi utakaowafanya wasisubiri kuajiriwa bali wajiajiri wenyewe na kukuza biashara zao.