R Kelly anashikiliwa na polisi kwa unyanyasaji wa kingono

Muktasari:

Ni kufuatia tuhuma za kufanya ngono na mabinti wadogo

Chicago. Hatimaye tuhuma za unyanyasaji wa kingono zimempeleka lupango mwanamuziki R Kelly baada ya kufunguliwa mashtaka 10 katika jimbo la Chicago nchini Marekani.

R Kelly mwenye umri wa miaka 52, alijisalimisha polisi baada kufunguliwa mashtaka na wanawake ambao idadi yake haijawekwa wazi.

Kushikiliwa kwa mwanamuziki huyo kunakuja wiki kadhaa baada ya jarida la Surviving R Kelly kutolewa mabinti mbalimbali wakieleza namna staa huyo alivyokuwa akiwatumikisha kingono.

Staa huyo wa R&B ambaye jina lake halisi ni Robert Sylvester Kelly, amekuwa akituhumiwa kuwatumikisha kingono mabinti wadogo kwa zaidi ya muongo mmoja.

Mwanasheria wake, Steve Greenberg ameuambia mtandao wa  Associated Press kuwa mteja wake ameshtushwa na tuhuma zinazotolewa dhidi yake kwa kuwa hana hatia.