RC Chalamila ataka viongozi kuacha ubabaishaji

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Albert Chalamila (mwenye kofia), Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika (kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya  Wilaya ya Mbeya, Steven Katembo wakikagua maendeleo ya ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbeya Leo asubuhi. Ujenzi wa Hospitali hiyo umegharimu Sh1.5 bilioni na unatarajia kukamilika kabla ya Juni 30 mwaka huu. Picha na Godfrey Kahango

Muktasari:

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema viongozi waliopewa dhamana kuisimamia Serikali wakiacha ubabaishaji na kuendekeza rushwa na ufisadi, dhamira ya Rais John Magufuli kuwapatia huduma nzuri wananchi itafanikiwa


Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila amesema viongozi waliopewa dhamana kuisimamia Serikali wakiacha ubabaishaji na kuendekeza rushwa na ufisadi, dhamira ya Rais John Magufuli kuwapatia huduma nzuri wananchi itafanikiwa.

Chalamila ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 12, 2019 baada ya kukagua ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Mbeya inayojengwa eneo la Inyala huku akiridhishwa na kasi ya ujenzi huo uliogharimu Sh1.5 bilioni.

“Magufuli ana dhamira  nzuri na kubwa kwa Watanzania. Lakini niseme sisi viongozi aliotuamini tukiwa ‘wasanii’ katika kutekeleza maazimio yake hatutamuwakilisha vizuri.”

“Lakini tukiacha ‘usanii’  na kuweka kando ufisadi na rushwa tutamwakilisha vyema katika kuwahudumia wananchi wetu,” amesema Chalamila.

Amebainisha ujenzi wa hospitali tatu za Wilaya ya Mbarali, Busokelo na Mbeya pamoja na vituo vya afya 14 utagharimu zaidi ya Sh6 bilioni, kubainisha kuwa unaendana na agizo la Serikali kutaka hospitali zote ziwe zimekamilika kabla ya Juni 30, 2019.

Mkurugenzi mtendaji Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Steven Katembo amesema kiasi hicho cha fedha kimetumika kujenga majengo saba ya hospitali hiyo lakini Sh60 milioni zilitolewa na halmashauri yake zimejenga majengo mengine mawili ambayo ni nyumba za watumishi.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Paul Ntinika amesema kukamilika na kuanza kutumika hospitali hiyo itakuwa msaada mkubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.