RC Mghwira ahubiri, azungumzia waumini kwenda makanisa ‘ya kiroho’

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira

Muktasari:

 

  • Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, leo Jumapili Machi 24, 2019  wametoa mahubiri mazito kwa waumini wa Kikristo nchini

Moshi. Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Anna Mghwira na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Fredrick Shoo, leo Jumapili Machi 24, 2019  wametoa mahubiri mazito kwa waumini wa Kikristo nchini.

Wawili hao wamekutana katika ibada ya kwanza asubuhi katika usharika wa Moshi Mjini  Dayosisi ya Kaskazini  katika maadhimisho ya miaka 25 ya kikundi cha wanawake cha Tabitha.

Katika mahubiri yake,  Mghwira aliyewahi kuwa mchungaji wa KKKT amesema makanisa ya kihistoria nchini yameanza kupoteza mvuto kutokana na baadhi ya waumini kuchoshwa na liturujia ya makanisa hayo.

Amesema waumini wengi siku hizi wanakwenda katika makanisa hayo kwa ajili ya kutafuta kuzikwa, kufungishwa ndoa na taratibu nyingine za kanisa.

"Liturujia zimeanza kukimbiza Wakristo kwenye makanisa haya makubwa ya kihistoria, wanakwenda huko asubuhi na baadaye mchana wanakwenda kwenye makanisa wanayoyaita ya kiroho,” amesema Mghwira na kuongeza:

"Baba askofu (Shoo) tunaomba utusaidie, uongozi wa kanisa unahitaji kurejesha huduma yake kikamilifu kwa waumini.

“Tunapojisikia kiu ya neno la Mungu, tunahitaji turudi hapa tunapotafuta maelekezo na urejesho wa mizizi ya imani turudi nyumbani, kwani tunapoanza kwenda kutafuta kushibishwa kiroho baada ya kupitia hapa asubuhi, maana yake kuna kitu kinapelea.”

Amesema katika siku hii ya wanawake wanamkumbuka mwanamke Tabitha alivyofanya matendo yaliyokuwa yakihitajika kwa wakati wake, hivyo kama ni viongozi au wachungaji wawafundishe waumini wao vya kutosha.

"Tabitha alionyesha wema wa matendo kwa watu aliotumwa kuwahudumia, wewe na mimi tujiulize tumetumwa kwa nani leo, kama ni mchungaji tufundishe vya kutosha na tutumie muda mwingi kuandaa na kutafuta kusikia kutoka kwenye sauti ya Mungu mwenyewe, kwamba hawa waumini wanahitaji nini ili wakija asubuhi wakitoka watoke na neno lililoshiba na wasiende kutafuta kushiba kwingine,” amesema.

Naye Dk Shoo amewatahadharisha waumini na makanisa mapya yanayoibuka na kudai kuwa makanisa makubwa ya kihistoria ni ya kizamani.

"Sio kila kitu kipya ni chema, kwa sasa kuna roho imeibuka ya kutaka vitu vipya, Wakristo naomba tujihadhari na roho hiyo, kwani mbinu zinazotumika ni zile za ibilisi  ambazo alizitumia katika Bustani ya Edeni," amesema Dk Shoo na kuongeza:

"Katika Bustani ya Edeni, Adam na Eva hawakukosa kitu lakini ibilisi alikuja na kuwalaghai, sasa wanakuja na kuwaambia makanisa yenu ni ya kizamani sana, Liturujia ni ya kizamani hakuna neno la Mungu, kule ni ya Kimwili siyo ya Kiroho, jihadharini sana."

Amesema ni vyema Wakristo wakawa waangalifu na kuacha kutapatapa na kudanganyika, kwani wameibuka mitume na manabii wa uwongo.

Kikundi cha wanawake cha Tabitha kilichopo chini ya idara ya Wanawake Dayosisi ya Kaskazini ya kanisa hilo, kimekuwa kikitoa huduma ya matendo ya huruma kwa wasiojiweza, yatima, wazee na wajane.