Raia wa Latvia adakwa na dawa za kulevya D’Salaam

Friday April 19 2019

 

By Pamela Chilongola,Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kikosi cha Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) limemkamata raia wa Latvia, Linda Mazure (22) akiwa na dawa za kulevya aina ya heroin zenye uzito wa kilo 5.091 alizokuwa akisafirisha kwenda Poland.

Kamanda wa Polisi Viwanja vya Ndege Tanzania, Jeremiah Shila alisema jana kwamba raia huyo alikamatwa juzi saa tisa alasiri katika uwanja huo akiwa ameficha dawa hizo katika mabegi mawili ya nguo.

Kamanda Shila alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa akiwa anajiandaa kwenda Poland kwa usafiri wa Shirika la Ndege la Qatar kupitia mji wa Doha.

Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa na hati ya kusafiria yenye namba LV5893769 iliyotolewa Aprili 6, 2018.

“Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa usalama uwanja wa JNIA walimkamata Linda akiwa eneo la abiria la ukaguzi wa awali Teminal II.”

Shila alisema raia huyo anaendelea kushikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi utakapokamilika atafikishwa mahakamani.

Advertisement

Pia alitoa onyo kwa watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, nyara za Serikali, utoroshaji wa madini na uharifu wa aina yeyote kwa kutumia viwanja vya ndege waache kwani wakibainika watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Oktoba 2, mwaka jana, Raia wa Brazili Candido De Oliverira(60) alikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(Kia) akiwa na unga unaodhaniwa ni dawa za kulevya wenye uzito wa kilo 6.1.

Kamishna wa Operesheni wa Mamlaka ya Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), Luteni Kanali Fredrick Milanzi Oktoba 3, aliwaambia waandishi wa habari kuwa walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa baada ya kudhibiti mianya waliyokuwa wanatumia kupitisha dawa hizo ambayo ni pamoja na viwanja vya ndege.

Advertisement