Rais: Jeshi lipewe zabuni

Rais  John  Magufuli akisalimiana na Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Phaustine Kasike baada ya kuwasili katika eneo la Mashamba ya Mahindi ya Gereza la Kilimo na Mifugo la Kitai lililopo Mbinga mkoani Ruvuma. Picha na Ikulu

Dar es Salaam/Ruvuma. Rais John Magufuli ametaka watendaji wa serikali kulitumia jeshi katika miradi ya dharura ili ifanyike kwa haraka na ufanisi.

Alisema hayo wakati wa kufungua kiwanda ambacho kina uwezo wa kusaga tani 20 za mahindi kwa saa 24, na hivyo kuwa na uwezo wa kuondoa tatizo mikoa ya kusini ambayo ni maarufu kwa kilimo cha nafaka.

Rais Magufuli aliyasema hayo jana wilayani Mbinga wakati akifungua kiwanda cha kuchakata mahindi kinachomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Tani 20 ni takriban theluthi mbili ya shehena ya lori moja (semi trailor).

Rais Magufuli, ambaye anaendelea na ziara katika mikoa ya kusini, alisema anafahamu kuwa kuna sheria ya manunuzi inayohusisha utangazaji wa zabuni, lakini akasema inatoa mwanya huo wa ununuzi wa dharura.

“Katika sheria hii kuna kazi ambazo huhitaji kutangaza. Daraja likikatika huwezi kutangaza. Sasa mtumie hizi kazi za dharura muwaweke wanajeshi,” alisema.

“Hata ukitaka kutengeneza kiwanda cha mahindi sema emergency (dharura), ukitaka kutengeneza barabara sema emergency. Sijasema kwamba tender (zabuni) zisitangazwe, lakini kama inawezekana kuchomekeachomeka tu. Itasaidia vijana wetu kupata ajira.”

Kifungu cha 65 cha Sheria ya Manunuzi ya Umma kinasema ofisa masurufu anaweza kufanya manunuzi ya aina hiyo iwapo ataona kufanya hivyo ni kwa masilahi ya umma katika masuala yanayotishia uhai, afya, usalama au kuwepo kwa majanga ya asili au kutishia kuendelea kufanya kazi kwa Serikali au taasisi inayotaka kufanya manunuzi.

Hata hivyo, sehemu zinazofuata zinaweka masharti ya jinsi ya kutekeleza manunuzi ya dharura, ikiwa ni pamoja na kuidhinishwa na wakala pamoja na mlipaji mkuu wa Serikali.

“Ukienda China na Misri kuna miji imejengwa na wanajeshi na sisi tunapaswa kubadilika. Wakati wa usalama, hakuna vita, ni lazima tuyatumie majeshi yetu kuimarisha miundombinu kwa sababu hata gharama ni ndogo lakini hata fedha zikienda huko zitawasaidia,” alisema.

“Waziri wa Nishati, kama kuna sehemu unataka kupeleka umeme kwa haraka, tumia jeshi likaweke nguzo huko na watu wapate nishati hiyo haraka. Kwa nini uhangaike kutangaza zabuni siku 45? Nasisitiza miradi ile ya haraka mtumie mbinu.

“Na nyie makamanda wa jeshi (JWTZ) na JKT mkisikia kuna kazi hizo za dharura ombeni haraka mkazifanye kwa sababu mnahusika na emergency. Hiyo itasaidia kupeleka nchi haraka.”

Alikuwa akifungua kiwanda cha kusaga nafaka kilichojengwa na kinachomilikiwa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT). Kiwanda hicho kina uwezo wa kusaga nafasi tani 20 kwa siku na hivyo kuwa sehemu ya suluhisho kwa wakazi wa mikoa ya Ruvuma, Mbeya, Rukwa, Iringa na Songwe, ambayo huzalisha nafaka kwa wingi.

“Ni matumaini yangu kuwa wakulima wa mahindi mkoani Ruvuma watapa soko la uhakika na jeshi litanunua mahindi hayo kwa bei nzuri,” alisema Rais.

Awali, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Venance Mabeyo alisema kiwanda hicho kitasaidia kutoa soko la kuaminika kwa wanaokizunguka kikosi cha JKT Mlale na mkoa mzima wa Ruvuma

Alisema soko la uhakika litasaidia kuongeza uzalishaji wa zao la mahindi kwa wakazi wa mkoa huo mahiri kwa kilimo cha zao hilo.

Jenerali Mabeyo alimuahidi Rais kuwa jeshi litaendelea kufanyia kazi maelekezo wanayopewa na wataendelea kuunga mkono juhudi za serikali za kujenga uchumi wa viwanda.