Breaking News

Rais Magufuli ampigia simu waziri Mbarawa mkutanoni, ampa maagizo

Thursday July 11 2019

 

By Baraka Samson, Mwananchi

Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli leo Alhamisi Julai 11, 2019 amempigia simu Waziri wa Maji, Profesa Makame Mbarawa akimtaka kuhakikisha maji yanapatikana katika mji wa Kyaka mkoani Kagera alikosimama kuzungumza na wananchi waliomueleza jinsi wanavyohaha kupata maji.

Baada ya kuelezwa kero hizo, kiongozi mkuu huyo wa nchi alichukua simu yake ya mkononi na kumpigia Profesa Mbarawa, kumuagiza kuwa mpaka Desemba, 2019 ahakikishe maji yanatoka katika eneo hilo.

“Kata pesa popote leta hapa nataka wananchi wa hapa washerehekee sikukuu ya Krismasi mwaka 2019 wakiwa na maji, sitaki mfanye upembuzi yakinifu kwa sababu ukiangalia hapa unaona kabisa maji yapo tu,” amesema Magufuli.

Huku akiweka simu karibu na kipaza sauti na mazungumzo yake na waziri huyo kusikika kupitia spika kubwa zilizokuwa katika moja ya magari yaliyopo katika msafara wake, Magufuli alimtaka Profesa Mbarawa awaeleze wananchi lini atafika Kyaka kuhakikisha maji yanapatikana.

Katika majibu yake,  Profesa Mbarawa amesema amepokea maagizo hayo na atafika Kyaka hivi karibuni kuanza kazi kama alivyoagizwa.

 

Advertisement

Advertisement