Rais Trump ashtakiwa Marekani

Tuesday February 19 2019
trumpypic

California, Marekani. Muungano wa majimbo 16 nchini Marekani yakiongozwa na California yameushtaki utawala wa Rais Donald Trump kuhusu uamuzi wa kutangaza hali ya dharura ili kukusanya fedha za ujenzi wa ukuta wa mpakani na Mexico.

Kesi hiyo imefunguliwa katika mahakama ya wilaya ya Kaskazini katika jimbo la California.

Hatua hiyo inakuja baada ya Trump kuidhinisha hali ya dharura, inayompa nguvu kulivuka Bunge na kujipatia fedha kwa ujenzi huo  ambao ni ahadi kubwa aliyoitoa wakati wa kampeni yake.

Chama cha rais huyo cha Republican kimedai kitahakikisha kinapinga hatua hiyo  kwa kutumia njia zozote zilizopo.

Mwanasheria mkuu jimbo hilo la California, Xavier Becerra amesema wanampeleka Trump mahakamani kuzuia matumizi mabaya ya nguvu za rais.

"Tunamshtaki Trump kumzuia dhidi ya kuiba pesa za mlipa ushuru, zilizotengwa kisheria na Bunge kwa watu wa majimbo yetu. Kwa wengi wetu, ofisi ya rais si eneo la vioja," aliongeza Becerra.

Advertisement

Kesi hiyo iliyofunguliwa Jumatatu inaanza kwa kusikilizwa awali ombi la kutaka kumzuia Trump ashughulikie dharura hiyo aliyoitangaza, wakati kesi ikiendelea kortini, gazeti la Washington Post linaripoti.

Trump alitangaza mpango huo baada ya Bunge kuukataa mpango wa ujenzi wa ukuta.

Ijumaa iliyopita kundi la kutetea raia, lilifungua kesi kwa niaba ya hifadhi asili, na wamiliki watatu wa ardhi katika jimbo la Texas ambao wamearifiwa huenda ukuta huo ukajengwa kwenye ardhi yao.

Akitoa tangazo hilo katika Ikulu ya White House siku ya Ijumaa, Trump amesema hali hiyo itaruhusu kupata takriban dola bilioni 8 kwa ujenzi wa ukuta huo wa mpakani.

Hiki ni kiwango kilicho chini ya gharama ya jumla ya dola bilioni 23 zinazohitajika kujenga ukuta huo wenye urefu wa maili 2000 wa mpakani.

Trump alikubali kwamba angeshtakiwa kwa hatua hiyo, na alitabiri kwamba kutangaza kwa hali hiyo ya dharura kutasababisha hatua za kisheria ambazo zina uwezekano mkubwa kuishia katika mahakama ya juu zaidi.

 

 


Advertisement