Rais ajipiga risasi kwa kupokea rushwa

Muktasari:

  • Ni baada ya kuona polisi wamefika nyumbani kwake kupata taarifa ya kutafutwa na polisi kwa tuhuma hizo

Lima,Peru. Rais wa zamani wa Peru, Alan García amejipiga risasi mwenyewe, baada ya kugundua kuwa anatafutwa na jeshi la polisi nchini humo kwa kosa la kupokea rushwa.

García anatuhumiwa kwa kupokea  rushwa kutoka kampuni ya ujenzi wa Brazil Odebrecht, ambapo amekuwa akizikataa tuhuma hizo mara kwa mara.

Luis Gonzales Posada, ambaye ni mmoja kati ya viongozi wa chama cha García, alisema  hali yake ni mbaya, “hebu tumuombee Mungu ampe nguvu,” aliwaambia waandishi wa habari waliofika hospitali.

García ambaye alikuwa Rais kuanzia mwaka 1985 hadi 1990 na kurudi madarakani tena mwaka 2006 hadi 2011 amekuwa rais wa  kwanza kutaka kujiua kwa tuhuma za kupokea rushwa.

Taarifa zilizotolewa na wachunguzi zinadai kuwa,  alipokea rushwa kutoka kwenye kampuni ya Ujenzi ya Brazili ya Odebrecht wakati wa kipindi cha pili cha Urais.

 Kampuni hiyo ilikubali kulipa zaidi ya Dola za Kimarekani 30milioni kama rushwa nchini Peru tangu 2004.

 Taarifa kutoka nchini humo zilisema kwamba rais huyo baada ya kujipiga risasi alikimbizwa hospitali ya Casimiro Ulloa hospital iliyopo mji mkuu wa Lima.

Taarifa zilisema kwamba alipata majeraha makubwa kichwani mwake yaliyosababishwa na risasi hizo ambazo alijimiminia  yeye mwenyewe.

Waziri wa Afya nchini humo Zulema Tomás alisema kwamba hali ya rais huyo ni mbaya sana, kwani alipata majeraha kichwani kwake.

“Tumuombee Mungu aweze kurudi katika hali yake ya kawaida kwani majeraha aliyoyapata ni makubwa sana’’ alisema mwanasheria wake Erasmo Reyna alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hospitalini hapo