Ripoti zamulika nafasi ya mwanamke SADC

Katibu Mtendaji wa SADC, Dk Stergomena Tax akizungumza wakati wa uzinduzi wa mapisho matano ya SADC leo jijini Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

 Ripoti hizo zinazotoa picha halisi katika nafasi ya mwanamke pamoja na mapendekezo, imezinduliwa leo Agosti 14, 2019 katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere(JNICC) ikiwa ni siku mbili tatu kabla ya kuanza kwa ratiba ya Mkutano Mkuu wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 16 za Jumuiya hiyo

Dar es Salaam. Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC), imekuja na mikakati mitano inayojikita katika kutazama nafasi ya mwanamke katika masuala ya ulinzi na usalama, maendeleo ya kiuchumi, nafasi za uongozi, ufuatiliaji wa sekta ya nishati na miundombinu.

Ripoti hizo zinazotoa picha halisi katika nafasi ya mwanamke pamoja na mapendekezo, imezinduliwa leo Agosti 14, 2019 katika Kituo cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), ikiwa ni siku mbili tatu kabla ya kuanza kwa ratiba ya Mkutano Mkuu wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi 16 za Jumuiya hiyo.

Ripoti ya kwanza ni Mkakati wa Wanawake katika ushiriki wa masuala ya ulinzi na usalama ndani ya SADC, Mkakati wa ufuatiliaji wa Maendeleo ya Jinsia wa SADC, Mpango wa Kushughulikia ukatili wa kijinsia katika SADC, Mpango wa ufuatiliaji sekta ya Nishati na Tathmini ya Mpango mfupi ya uendelezaji miundombinu.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti hizo, Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Dk Stergomena Tax amesema kwa miaka mingi changamoto za ulinzi na usalama zinapotokea zimekuwa zikiathiri kila kundi huku mwanamke akiwekwa kando, jambo ambalo haliwezi kufanikisha upatikanaji wa suluhu.

“Kuhusu tathmini ya maendeleo ya kijinsia, utaangaliwa uko kwa namna gani, tathmini imeonyesha sera zimehusishwa kikanda, kitaifa lakini bado hatuwezi kusema kwamba kuna fursa sawa za kiuchumi na hata kisiasa, tukiongeleza siasa ni 50 kwa 50 ila hadi sasa kuna nchi mbili tu kati ya 16 zilizofikia bunge, ambazo ni Afrika kusini,” amesema.

 “Kwa hiyo mkakati umeainisha ni wapi tumefanya vizuri, wapi tunahitaji jitihada zaidi, nini kifanyike.”