Rita kuhakiki vyeti vya vifo, kuzaliwa kwa wanafunzi

Ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Emmy Hudson

Muktasari:

  • Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) imesema ucheleweshwaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu unachangiwa na wanafunzi wenyewe kwa kuchelewa kuhakiki taarifa zao hivyo imewataka kufanya uhakiki mapema.

Dar es Salaam. Ofisa mtendaji mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Emmy Hudson amewataka wanafunzi wa elimu ya juu nchini kufanya uhakiki wa vyeti vya vifo na kuzaliwa mapema ili kuepuka usumbufu ikiwemo kucheleweshewa mikopo.

Wanafunzi hao ni wale wanaotarajia kuwasilisha maombi ya mikopo ya elimu ya juu inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) kwa mwaka 2019/ 2020.

Akizungumza leo Jumanne, Aprili 23, 2019, Emmy amesema uhakiki huo unaoanza rasmi leo unalenga kutatua changamoto na malalamiko kwa wanafunzi kukosa mikopo.

“Kwa hiyo milango ipo wazi, wasisubiri hatua za mwisho wakaishia kuilalamikia Bodi ya Mikopo kuwa wamewacheleweshea mikopo,” amesema.

Amesema jumla ya wanafunzi  98,000 kati ya 100,800 waliopeleka maombi yao mwaka jana nyaraka zao zilikuwa halali huku wanafunzi 2,000 nyaraka zao zilibainika kutokuwa kwenye mfumo rasmi.

“Kwa mwanafunzi anayeleta maombi yake atapatiwa majibu baada ya siku tatu, hivyo kuanzia leo aingie katika mtandao kwa anuani: uhakiki.rita.go.tz/uhakiki.