SSRA kaa la moto

Dar. Kuna kila dalili kuwa Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Jamii (SSRA) imevunjwa na wafanyakazi wake wametawanywa kwenye idara nyingine za Serikali, Mwananchi limebaini.

Hatua hiyo imekuja miezi saba tangu Rais John Magufuli alipotengua uteuzi wa aliyekuwa mkurugenzi wake mkuu, Dk Irene Isaka na kumteua Onorius Njole kukaimu nafasi yake.

Taarifa zilizolifikia Mwananchi kwa karibu mwezi sasa, zinaonyesha kuwa mamlaka hiyo imefunga ofisi zake za makao makuu zilizopo eneo la Victoria, Barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam.

Mwandishi wetu aliyefika katika jengo la ofisi hizo alikuta zimefungwa.

Mlinzi wa Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) aliyekuwa akilinda eneo hilo na ambaye hakutaka kutaja jina lake alisema ofisi hizo zilifungwa tangu Julai Mosi.

“Hapa wafanyakazi wote wameshaondoka, kama una shida nao nenda Wizara ya Kazi na Ajira,” alisema.

Mlinzi mwingine alisema kuondoka kwa wafanyakazi hao kulikuja ghafla kwani wengi hawakuwa na taarifa.

“Wafanyakazi wametawanywa kwenye ofisi mbalimbali za Serikali, wengine kwenye benki na mifuko ya pensheni iliyopo,” alisema mlinzi huyo ambaye pia hakutaka kutaja jina lake.

Alipotafutwa kuzungumzia suala hilo, mkuu wa kitengo cha uhusiano na uhamasishaji wa SSRA, Sarah Kibonde alieleza kuwa amehama na kumwelekeza mwandishi kumtafuta katibu mkuu ofisi ya Waziri Mkuu, “nilikuwa mtumishi wa eneo hilo, lakini sasa niko eneo jingine huko sihusiki.”

Alipotafutwa, ofisa habari wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Agustino Tendwa alisema mtu pekee anayeweza kulisemea jambo hilo ni Katibu Mkuu na kumtaka mwandishi kuwasiliana na ofisa habari anayeshughulika na kitengo hicho, Ridhiwan Wema ambaye hata hivyo, ilielezewa kwamba amehamishiwa mkoani Njombe.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, anayeshughulikia Kazi, Ajira na Vijana, Andrew Massawe hakupatikana kwani mwandishi wetu alifika ofisini kwani mara mbili lakini hakufanikiwa kuonana naye akielezwa kuwa katika kazi nyingine na hata alipopigiwa simu yake ya mkononi iliita bila majibu.

Mwananchi pia lilimtafuta Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Anthony Mavunde ambaye alisema masuala yanayohusu wizara hiyo msemaji wake ni mmoja tu waziri mwenye dhamana ambaye ni Jenista Mhagama.

Mwandishi wetu alimtafuta kwa simu Waziri Mhagama bila mafanikio na juzi alikwenda ofisini kwake Mtumba nje kidogo ya jiji la Dodoma na kuelelezwa kuwa ametoka.

Jana, alifika tena ofisini kwa waziri huyo na kuambiwa kuwa ametoka nje ya ofisi, lakini amsubiri atarudi.

Baada ya kumsubiri kwa muda mrefu, alitakiwa kuacha maelezo ya jambo analohitaji ufafanuzi wake.

Baadaye alimpata Waziri Mhagama kwa simu na baada ya kumuuliza kuhusu taarifa za kuvunjwa kwa SSRA alijibu, “masuala ya kazi njoo ofisini. Siko Dodoma niko safarini nitakapokuwa nimerudi ofisini nitakutafuta.”

Majukumu ya SSRA yalianza kupungua baada ya sheria ya kuanzishwa mfuko wa PSSSF unaoshughulikia sekta ya umma kusainiwa Februari 8 na kufuatiwa na kukamilika kwa mchakato wa kuvunjwa kwa mifuko ya PPF, GEPF, LAPF na PSPF kwa watumishi wa umma, huku kwa sekta binafsi ukibaki mfuko wa NSSF. Pia, ilikuwa ikiratibu shughuli za mifuko ya bima ya afya, fidia na hiari.

Moja ya mambo ya kukumbukwa ya taasisi hiyo ni jinsi ilivyoshughulikia mabadiliko ya kikokotoo cha wastaafu, mchakato ambao ulisababisha mvutano mkubwa baina yake na wafanyakazi.

Mbali ya wafanyakazi, waziri kivuli anayeshughulikia kazi, Ester Bulaya alikosoa mabadiliko hayo.

Mvutano huo ulimfanya Rais Magufuli kuitisha mkutano Desemba 28, 2018 na viongozi wa Tucta, watendaji wakuu wa PSSSF, NSSF na SSRA kujadili mvutano huo uliotokana na mabadiliko ya sheria ya mafao ambayo ilileta ukokotoaji mpya kwa watumishi wa umma.

Wakati SSRA ikisisitiza kuwa lengo la kubadili kikokotoo lilikuwa kuwafanya wastaafu wanufaike zaidi kama ilivyokuwa kabla ya sheria mpya, wafanyakazi walipinga wakisema kinawapunja wastaafu fedha ya mkupuo.

Rais Magufuli aliamua kwamba kikokotoo kilichokuwa kinatumiwa awali kiendelee hadi mwaka 2023. Muda mfupi baada ya mkutano huo, alitangaza kutengua uteuzi wa Dk Isaka.